• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Huyu ‘Iniesta’ wa Nzoia ni hatari kwa pasi za maangamizi

Huyu ‘Iniesta’ wa Nzoia ni hatari kwa pasi za maangamizi

NA CECIL ODONGO

NZOIA Sugar ni kati ya timu ambazo zimeshangaza wengi msimu huu kutokana na jinsi ambavyo inafanya vyema katika Ligi Kuu (KPL).

Baada ya kuwajibikia mechi sita, Nzoia ambao walitwaa ubingwa wa KPL mnamo 2002, inashikilia nafasi ya pili kwa alama 13 baada ya mitanange sita.

Timu hiyo inayofundishwa na Kocha Salim Babu imetenganishwa na viongozi Tusker kwa alama mbili pekee katika msimamo wa jedwali.

Kando na hayo, Nzoia imejizolea sifa chekwachekwa kutokana na jinsi ambavyo inacheza mpira wa migusomiguso, mtindo ambao umezoeleka kwa timu za taifa za Uhispania na Brazil pamoja na klabu za Arsenal na Barcelona.

Mwanadimba mahiri ambaye amekuwa injini na kuisaidia kupata matokeo hayo mazuri ni kiungo Boniface ‘Iniesta’ Munyendo.

Kiungo huyo amekuwa akiwaburudisha mashabiki kutokana na uwezo wake wa kuumiliki mpira kisha kuwavuta mabeki wa timu pinzani kabla ya kutoa pasi zilizoenda ‘shule’ kwa wenzake timuni.

Katika safu ya Nzoia, ushirikiano wake na kiungo wa Harambee Stars, Kevin Juma, umesifiwa sana na mashabiki kama kiini cha ufanisi ambao Nzoia imepata hadi sasa KPL.

Iwapo Nzoia hawana mshambuliaji basi hamna tatizo kwa kuwa Munyendo anaweza kupangwa mbele awe ‘false nine’.

Licha ya kuendelea kung’aa kwa Wanasukari hao, huu ndio msimu wa pili ambapo kiungo huyo anashiriki KPL kwa kuwa msimu jana alikuwa Vihiga Bullets.

Kufikia sasa Munyendo amecheka na nyavu za wapinzani mara nne na anaongozo orodha ya wafungaji akiwa pamoja na Benson Omala (Gor Mahia) na Mganda anayesakatia Tusker Deogratious Ojok.

Kinaya ni kwamba Omala na Ojok ni washambuliaji huku Munyendo akiwa kiungo.

Hata hivyo, mabao yake yote yametokana na mikwaju ya penalti.

Munyendo alifunga penalti mbili katika ushindi wa 2-1 dhidi ya KCB mnamo Disemba 11, na pia 1-0 dhidi ya Nairobi City Stars Disemba 17.

Mnamo Disemba 22 alifunga penalti kwa mara nyingine walipoilemea Mathare United 2-1 ugani Ruaraka.

“Japo mabao yangu yametokana na mikwaju ya penalti, yalitusaidia kupata ushindi. Kufunga penalti pia kunahitaji ustadi mkubwa,” akasema mwanadimba huyo.

“Sikuamini kuwa ningeanza vyema KPL. Kando na magoli nimekuwa nikizalisha pasi ambazo zimeishia kufungwa na wenzangu. Najituma sana ila kucheza soka inayoburudisha pia hunipa raha hasa pasi nyingi kutoka lango letu hadi lango jingine,” akaongeza.

Akiwa na umri wa miaka 22, Munyendo anasema hajashangazwa na ustadi wake kiasi cha kuaminiwa kupiga penalti kwenye mechi kalikali.

  • Tags

You can share this post!

NYOTA WA WIKI: Miguel Almiron

Jagina Pele, aliyewahi kuzuru Kenya, atazikwa Jumanne

T L