• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Jeraha la goti kumnyima Paul Pogba fursa ya kuongoza Ufaransa kutetea ubingwa wa Kombe la Dunia nchini Qatar

Jeraha la goti kumnyima Paul Pogba fursa ya kuongoza Ufaransa kutetea ubingwa wa Kombe la Dunia nchini Qatar

Na MASHIRIKA

KIUNGO matata wa Juventus, Paul Pogba, atakosa kuongoza timu ya taifa ya Ufaransa kutetea Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka huu 2022 kutokana na jeraha la goti.

Pogba, 29, hajachezea Juventus ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) pambano lolote msimu huu tangu ajiunge upya na kikosi hicho baada ya kuagana na Manchester United mnamo Julai 2022.

Alipata jeraha baya la goti mnamo Julai na akahiari kutofanyiwa upasuaji kwa matumaini kuwa angekuwa amepona kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa fainali za Kombe la Dunia kupulizwa.

Ufaransa waliokomoa Croatia 4-2 na kutwaa Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi, watafungua kipute cha mwaka huu dhidi ya Australia mnamo Novemba 22, 2022.

Kwa mujibu wa taarifa ya Rafaela Pimenta ambaye ni wakala wa Pogba, tathmini ambazo sogora huyo alifanyiwa Oktoba 30 na 31, 2022 mjini Torino na Pittsburgh zilibainisha kuwa Pogba anahitaji muda zaidi wa kupona baada ya kufanyiwa upasuaji kwenye goti.

Pogba aliwajibikia Ufaransa mara ya mwisho mnamo Machi 2022 katika pambano la kirafiki lililowashuhudia wakitandika Afrika Kusini 5-0 kirafiki. Alirejea mazoezini mwanzoni mwa Septemba 2022 kabla ya kuhiari kufanyiwa upasuaji.

Baadaye, alisalia mkekani kwa kipindi kirefu na ilikuwa hadi wiki mbili zilizopita ambapo alipendekezewa aanze mazoezi mepesi kambini mwa Juventus.

Kwa mujibu wa ripoti kutoka Italia, Pogba alipata jeraha jingine la paja akishiriki mazoezi kambini mwa Juventus mnamo Oktoba 30, 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Samuel Njoroge sasa ndiye Karani mpya wa Bunge la Kitaifa

Kaunti ya Mombasa yashtakiwa na kampuni ya glasi

T L