• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Juventus kumwachilia Ronaldo kujiunga na Man-City au PSG kwa masharti yao

Juventus kumwachilia Ronaldo kujiunga na Man-City au PSG kwa masharti yao

Na MASHIRIKA

JUVENTUS wamemweleza Cristiano Ronaldo kwamba wako radhi kumtia mnadani muhula huu ila kwa masharti yao.

Nyota huyo raia wa Ureno mwenye umri wa miaka 36 angali na mwaka mmoja pekee kwenye mkataba wake wa sasa na Juventus ambao ni miamba wa soka ya Italia.

Mustakabali wa Ronaldo kitaaluma umekuwa ukimulikwa zaidi katika siku za hivi majuzi baada ya kuachwa nje ya kikosi cha kwanza kilochotegemewa na Juventus katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) muhula huu wa 2021-22 dhidi ya Udinese.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Italia, Jorge Mendes ambaye ni wakala wa Ronaldo, amezungumza na baadhi ya vikosi maarufu vya bara Ulaya kuhusu uwezekano wa kumsajili Ronaldo ambaye anamezewa pakubwa na Manchester City na Paris Saint-Germain (PSG).

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City wanahemea maarifa ya Ronaldo ili ajaze pengo la fowadi Sergio Aguero aliyeyoyomea Uhispania mwishoni mwa msimu wa 2020-21 kuvalia jezi za Barcelona.

Man-City wanaanza kuhemea maarifa ya Ronaldo baada ya juhudi zao za kumtwaa nahodha na fowadi wa Tottenham Hotspur, Harry Kane, kuzaa nunge.

Mendes tayari amewafichulia Juventus kuhusu mpango wa kufanikisha mchakato wa kuondoka kwa Ronaldo jijini Turin, Italia baada ya kukutana na baadhi ya vinara wa Juventus wakiwemo Pavel Nedved (Makamu wa Rais), Maurizio Arrivabene (Afisa Mkuu Mtendaji) na Federico Cherubini (Mkurugenzi wa Soka).

Juventus waliweka mezani kima cha Sh15.5 bilioni miaka mitatu iliyopita ili kumshawishi Ronaldo kuagana na Real Madrid ya Uhispania.

Kubwa zaidi ambalo Mendes amefichua kwamba linamsukuma Ronaldo kuondoka Juventus ni kutofaulu kwa kikosi hicho kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) tangu mwanasoka huyo wa zamani wa Manchester United ajiunge nao. Licha ya kujivunia huduma za Ronaldo, Juventus wameshindwa kusonga mbele zaidi ya hatua ya robo-fainali za kipute hicho huku wakipigwa kwenye hatua ya 16-bora katika kipindi cha misimu miwili iliyopita.

Mnamo 2020-21, Juventus walishindwa kuhifadhi taji la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) walilolitia kapuni kwa miaka tisa mfululizo. Hiyo ni baada ya ukiritimba wao katika Serie A kukomeshwa na Inter Milan walioongozwa na kocha Antonio Conte kunyanyua taji hilo kwa mara ya kwanza tangu 2009-10.

PSG wamefichua pia azma ya kumsajili Ronaldo iwapo fowadi mahiri raia wa Ufaransa, Kylian Mbappe atayoyomea Uhispania kuvalia jezi za Real.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Pendekezo wabunge wapitishe ‘matunda’...

Askofu akubali kumtunza mtoto wa kambo