• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Pendekezo wabunge wapitishe ‘matunda’ yaliyobebwa ndani ya kapu la BBI

Pendekezo wabunge wapitishe ‘matunda’ yaliyobebwa ndani ya kapu la BBI

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya mswada kuwasilishwa bungeni ili kupitisha mambo muhimu yaliyotupiliwa mbali mahakama ya rufaa, ilipotupilia mbali mpango wa kubadilisha Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI).

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, alisema pendekezo hilo linazingatia maslahi ya mwananchi.

Alisema sasa ndiyo wakati mwafaka wa wabunge kutathmini maswala hayo kwa makini na kuona ya kwamba wanapitisha hayo bungeni ili “mwananchi wa kawaida aweze kunufaika pakubwa.”

Mbunge huyo aliyasema hayo Jumatano mjini Thika baada ya uamuzi wa majaji saba wa mahakama ya rufaa kutupilia mbali mswada wa BBI uliofikishwa mbele yao wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, baadhi ya maswala muhimu yaliyokuwa kwenye ripoti ya BBI yalikuwa ni kuongeza fedha za mgao kutoka asilimia 15 hadi 35 kwa kaunti.

Jambo lingine muhimu ni la kuongeza maeneobunge zaidi 70.

Eneo la Thika lilitarajia kugawanywa mara mbili huku Kaunti ya Kiambu ikiwa na viti sita zaidi.

Alieleza kuwa BBI ilikuwa muhimu sana kwa eneo la Mlima Kenya.

Mbunge huyo aliwahimiza viongozi popote walipo wawe mstari wa mbele kuwatetea wananchi badala ya siasa za malumbano.

“Hata wananchi wenyewe wako macho na wanajua vizuri viongozi wachapa kazi na wenye kupiga siasa bila maendeleo. Kwa hivyo mwaka ujao wa uchaguzi kila kiongozi atajua mbivu na mbichi,” alifafanua mbunge huyo.

Alipongeza juhudi za viongozi wa Mlima Kenya ambao ni Bw Mwangi Kiunjuri wa The Service Party (TSP), Martha Katia (Narc Kenya), na Moses Kuria wa Chama cha Kazi, kujitahidi kuileta pamoja jamii ya Mlima Kenya.

You can share this post!

Polisi sita wapinga kushtakiwa kwa mauaji

Juventus kumwachilia Ronaldo kujiunga na Man-City au PSG...