• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 5:50 AM
Kangemi Ladies wavamiwa na Nakuru City Queens ligini KWPL

Kangemi Ladies wavamiwa na Nakuru City Queens ligini KWPL

NA AREGE RUTH

KANGEMI Ladies walipata kipigo cha nne mtawalia msimu huu, waliponyeshewa 4-0 na Nakuru City Queens kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) katika uga wa Maonyesho ya Kilimo (ASK) mjini Nakuru.

Elizabeth Muteshi alifunga mabao mawili katika dakika ya 17 na 66 mtawalia nao viungo Stellah Mulongo na Melon Mulindi wakafunga bao kila mmoja dakika ya 58 na 84 mtawalia.

Muteshi aliingia kwenye orodha ya wafungaji bora msimu huu akiwa na mabao manne. Kwenye mechi ya awali, alifunga mabao mawili na kuchangia ushindi wa (5-1) dhidi ya Kayole Ladies wikendi iliyopita.

Kwenye mechi za awali nne, Nakuru walitoka sare ya (0-0) dhidi ya Gaspo Women, (1-0) dhidi ya Kisumu All Starlets, walilala mikononi mwa Thika Queens ambao waliwanyorosha (4-1), wakaamuka na Kayole Ladies kwa kuwakung’uta (5-1).

Nakuru walipanda hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 10 sawa na wanajeshi wa Ulinzi Starlets. Alama tatu nyuma ya viongozi wa ligi Vihiga Queens.

Meneja wa klabu hiyo Bernard Efitoko anasema,”Ilikuwa ni mechi ngumu hata ingawa tulipata ushindi. Tulipoteza nafasi za wazi za kufunga mabao zaidi. Kwa ligi akuna mnyonge ukija vibaya utakanyagwa tu.”

Kati ya mechi tano za ligi ambazo Kangemi wamecheza msimu huu, wamefungwa jumla ya mabao 26.

Mechi ya kwanza ya ligi walipigwa (12-0) na Vihiga, Gaspo Women waliwanyorosha (4-0), wakapata alama za bure dhidi ya Kayole Ladies na kuvamiwa na Zetech Sparks ambao waliawaadhibu (6-1).

Kangemi wanachungulia kushuka daraja wakiwa nafasi ya 11 kwenye jedwali na alama tatu. Alama hizo tatu walipata bila kutolea jasho kutoka kwa Kayole ambao walisusia kucheza mechi hiyo uwanjani Camp Toyoyo wiki mbili zilizopita.

Mechi kati ya Gaspo Women na Kayole Ladies iliyopangwa kuchezwa katika uwanja wa Gems Cambridge maeneo ya Ongata Rongai kaunti ya Kajiado, iliahirishwa hadi Februari 1, 2023.
  • Tags

You can share this post!

Gavana Barasa alalama Khalwale amchafulia serikali

TALANTA: Kwaya wembe kwa kueneza Injili na kukuza vipawa...

T L