• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 11:30 AM
Watu watano wapoteza maisha kwenye ajali mjini Molo

Watu watano wapoteza maisha kwenye ajali mjini Molo

NA JOHN NJOROGE

WATU watano wamefariki kwenye ajali iliyowaacha wengine 10 wakiwa na majeraha baada ya matatu kugonga upande wa nyuma wa lori la trela kwenye barabara ya Molo-Kericho Jumamosi asubuhi katika eneo la Mau Summit.

Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi wa kaunti ndogo ya Kuresoi, Juddah Gathenge alisema wanaume wanne na mtoto walifariki papo wakati wa ajali hiyo iliyotokea saa tisa alfajiri.

Miili ya wahanga hao ilipelekwa katika hifadhi ya maiti ya kaunti ndogo ya Molo huku mabaki ya magari yakibururwa na kupelekwa hadi katika kituo cha polisi cha Mau Summit

“Magari yote mawili yalikuwa yakielekea Nakuru kutoka Kericho kabla ya matatu kubingiria mara kadhaa baada ya kugonga lori kutoka upande wa nyuma. Hatujabaini mara moja ikiwa matatu hiyo ilikuwa ikienda kwa kasi au kuvuka ajali hiyo ilipotokea lakini tumeanzisha uchunguzi,” akasema Bw Gathenge, akiongeza kuwa waliojeruhiwa walipelekwa katika hospitali zilizoko Molo na Londiani.

Mgonjwa aliyekuwa katika hali mbaya zaidi amepelekwa katika hospitali ya Nakuru CGH.

Akizungumza na Taifa Leo kwa njia ya simu, mkuu huyo wa polisi alitoa wito kwa madereva kuwa waangalifu zaidi hasa wanapoendesha magari usiku.

“Tunawaomba madereva wa magari wawe waangalifu hasa wakati huu tunapokaribia msimu sherehe za Krismasi. Pia hawafai kubeba abiria kupita kiasi, kupita mwendo kasi au kupita mahali ambapo barabara haieleweki,” alisema Bw Gathenge na kuongeza kuwa chanzo kikuu cha ajali barabarani ni madereva kukosa umakinifu.

Alisema madereva wa magari hawapaswi kunywa pombe na kuendesha magari ili kuepusha ajali za barabarani.

Ajali ya Jumamosi inajiri wiki chache tu baada ya takriban watu 10 kuangamia katika ajali ya barabarani karibu na kituo cha kibiashara cha Sobea katika barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.

  • Tags

You can share this post!

Mto Tana wavunja kingo mafuriko yakitatiza shughuli za...

Kenya kuvaana na Ufaransa mashindano ya Rugby League jijini...

T L