• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Mpira wa Vikapu: Kenya Morans yaanza maandalizi ya Kombe la Afrika

Mpira wa Vikapu: Kenya Morans yaanza maandalizi ya Kombe la Afrika

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya mpira wa vikapu ya wanaume ya Kenya maarufu kama Morans, itaanza maandalizi ya Kombe la Afrika (AfroBasket) hapo Julai 19.

Katibu wa Shirikisho la Mpira wa Vikapu Kenya (KBF) Andrew Kisoi alieleza Taifa Leo mnamo Ijumaa kuwa vijana hao wa kocha Liz Mills wataanzia shughuli yao katika ukumbi wa kitaifa wa Nyayo.

Morans ilijikatia tiketi ya kushiriki mashindano kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1993 kwa kuduwaza miamba Angola 74-73 katika mojawapo ya mechi zake za makundi za raundi ya mwisho jijini Yaounde, Cameroon mwezi Februari 2021.

Nyota Tylor Ongwae, ambaye tayari yuko nchini kutoka Denmark, alifunga alama mbili za mwisho katika sekunde ya mwisho zilizowezesha Kenya kubwaga Angola.

Morans ilipepeta Eritrea 112-64, Tanzania 95-59, Somalia 102-77, Burundi 101-83 na Sudan Kusini 74-68 katika mechi za Zoni ya Tano mwezi Januari 2020.

Kisha, ilizimwa na Senegal 92-54 na Angola 75-52 na kuchapa Msumbiji 79-62 katika Kundi B la raundi ya kwanza ya awamu ya mwisho ya kufuzu kushiriki AfroBasket mwezi Novemba 2020.

Katika raundi ya pili na mwisho ya awamu ya mwisho ya kujikatia tiketi ya AfroBasket, Morans ilipoteza 69-51 dhidi ya Senegal, ikalemea Angola 74-73 kabla ya kupigwa 71-44 na Msumbiji.

Vijana wa Mills walikuwa wamefanya ya kutosha kufuzu pamoja na Senegal iliyoshinda kundi hilo na nambari mbili Angola, huku Msumbiji ikibanduliwa.

AfroBasket ya wanaume itaandaliwa jijini Kigali nchini Rwanda kutoka Agosti 24 hadi Septemba 5. Morans wako katika kundi ngumu.

Makundi ya AfroBasket (wanaume): A – Rwanda, DR Congo, Angola, Cape Verde; B – Tunisia, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Misri, Guinea; C – Nigeria, Ivory Coast, Kenya, Mali; D – Senegal, Cameroon, Sudan Kusini, Uganda.

You can share this post!

Wanahandiboli Cereals Board na Nairobi Water mawindoni...

Dimba mlimani