• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Wanahandiboli Cereals Board na Nairobi Water mawindoni kudumisha rekodi ya kutoshindwa

Wanahandiboli Cereals Board na Nairobi Water mawindoni kudumisha rekodi ya kutoshindwa

Na AGNES MAKHANDIA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Shirikisho la Handiboli Kenya (KHF) Cereals Board (wanaume) na Nairobi Water (wanawake) watajibwaga uwanjani Nyayo hapo Julai 17 wakilenga kudumisha rekodi zao za kutoshindwa.

Cereals itapepetana na Inspired, nayo Water imeratibiwa kumenyana na Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) katika menyu ya michuano sita itakayosakatwa Jumamosi.

Timu ya Cereals inakutana na Inspired ambayo itakuwa ikifungua msimu. Meneja wa timu ya Cereals, Edina Kasandi anasema kila pointi ni muhimu.

Kasandi alikiri kuwa hawajakuwa na muda mzuri wa kufanya mazoezi, lakini ana matumaini watavuna matokeo mema.

“Mchuano huu utaamua jinsi wapinzani wetu wataanza ligi na itakuwa muhimu kwao kama tu sisi kwa sababu tunalenga kuendelea kuandikisha matokeo mazuri. Kumbuka kuwa sisi ni mabingwa watetezi na tunafaa kuonyesha nia yetu ya mapema ya kutetea taji,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa.

Cereals ni ya sita kwenye jedwali kwa alama mbili baada ya kushinda mechi moja wamecheza.

Naye kocha Jack Ochieng amesema kuwa vipusa wake wa Water hawatadharau wapinzani wao ambao wamekuwa wakiimarika.

KU inashikilia nafasi ya saba kwa alama mbili kutokana na mechi tatu nayo Water inaongoza kwa alama nne baada ya kucheza mechi mbili.

“Kila mechi ni muhimu kwetu na tutatafuta kutia kapuni alama zote mbili,” alisema Ochieng, ambaye ni kocha mkuu wa timu ya taifa ya kinadada.

Kocha wa KU, Geoffrey Barasa alikiri kuwa mchuano huo utakuwa mgumu.

Ratiba (Julai 17 kuanzia saa tatu asubuhi):

Chuo Kikuu cha Strathmore vs Chuo Kikuu cha TUK (wanaume)

Generation vs Buccaneers (wanaume)

Nairobi Water vs Chuo Kikuu cha Kenyatta (wanawake)

NCPB vs Inspired (wanaume)

Nanyuki vs Amazon (wanawake)

GSU vs Tigers (wanaume).

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE 

You can share this post!

Wakazi wa South Ngariama walalamikia hali mbovu ya barabara

Mpira wa Vikapu: Kenya Morans yaanza maandalizi ya Kombe la...