• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 4:23 PM
Kenya U13 yaelekea Uingereza kwa raga za kimataifa za Rosslyn Park 7s

Kenya U13 yaelekea Uingereza kwa raga za kimataifa za Rosslyn Park 7s

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Kenya ya wanaraga wasiozidi umri wa miaka 13 almaarufu IAPS Kenya imeelekea Uingereza kwa mashindano ya kimataifa ya shule ya Rosslyn Park Sevens yatakayofanyika mjini London mnamo Machi 23.

Kwenye mashindano hayo ya wachezaji walio kati ya umri wa miaka 11 hadi 18, vijana wa kocha Jim Ross watavaana na Brighton College, Sedbergh Prep, Beaudesert Park, Mill Hill & Belmont na Lord Landsworth College katika kitengo cha umri wa miaka 13 ya Kundi E.

Akizungumza katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta kabla ya kusafiri, Ross alisema, “Nakosa maneno ya kukuambia msisimko tulionao kuingiza mashindanoni vijana hawa 12 waliojaa talanta kutoka shule 10. Tunasubiri kwa hamu kubwa kushiriki mashindano, mechi za kujipima nguvu na ziara yote nzima.”

“Hii ni fursa nzuri kwa wachezaji hawa kuonesha kile wanaweza kufanya katika ulingo wa kimataifa. Mashindano haya ni nguzo moja ya kutengeneza programu ya chipukizi,” aliongeza Ross.

IAPS Kenya imeshiriki Rosslyn Park Sevens tangu 2012-2013, ikifanikiwa kukuza talanta iliyoishia kuchezea timu ya taifa ya Kenya. Baadhi ya wachezaji waliopitia katika mashindano hayo na kuchezea timu ya taifa ya Kenya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 almaarufu Chipu ama ile ya watu wazima Simbas ni Michele Brighetti, Dominic Coulson, Mark Mutuku, Jeff Mutuku, Owain Ashley, George Kyriazi na Josh Weru. Brighetti alinyakuliwa na Italia mwaka 2020 baada ya kuchezea Chipu.

Teshen Waire ndiye nahodha wa kikosi cha mwaka huu kilicho na mtoto wa mchezaji wa zamani wa klabu ya Mean Machine na Kenya Andrew Lopokoiyit, Sotei Lopokoyit, pamoja na Ogwe Ng’ong’a ambaye baba yake Edwin, alichezea shule ya Lenana pamoja na Mean Machine, Kenya na klabu ya Uingereza ya Blackheath RFC.

Mchezaji wa KCB RFC, Michael Wanjala, atasaidia benchi ya IAPS Kenya kwenye mashindano hayo yanayovutia zaidi ya wachezaji 10,000 kila mwaka.

Kikosi cha Kenya U13 IAPS:

Teshen Waire (Banda, nahodha), Sotei Lopokoiyit (Brookehouse, nahodha msaidizi), Ogwe Ng’ong’a (Banda), Nathan Van Aswegen (Banda), Toby Glen (Banda), Jack Foxton (Pembroke House), Archie Camm (Pembroke House), Lionel Lawrence (Pembroke House), Essein Lewis (BGE), Nana Epoku Nyame (Peponi House), Jayden Collis (Kenton College), Zachary Rusagara (Kenton College). Kocha mkuu – Jim Ross (Peponi House), manaibu wa kocha – Cameron Roberts (Banda), Michael Wanjala (Peponi House).

  • Tags

You can share this post!

Omanyala, Shelly-Ann Fraser-Pryce tayari kufyatuka kasi ya...

DOUGLAS MUTUA: Jumatatu si sikukuu rasmi

T L