• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
Kenya yaambulia patupu marathon ya wanawake jijini Budapest

Kenya yaambulia patupu marathon ya wanawake jijini Budapest

Na GEOFFREY ANENE

KWA mara ya kwanza katika makala saba Kenya imetoka mikono mitupu katika mbio za kilomita 42 za wanawake kwenye Riadha za Dunia jijini Budapest, Hungary, Jumamosi.

Kenya ilifagia medali za mwaka 2011 kupitia kwa Edna Kiplagat, Priscah Jeptoo na Sharon Cherop, ikapata dhahabu kupitia kwa Kiplagat mwaka 2013, fedha mwaka 2015 na 2017 kupitia kwa Helah Kiprop na Kiplagat mtawalia, dhahabu kutoka kwa Ruth Chepng’etich mwaka 2019 na fedha kutoka kwa Judith Korir mwaka 2022.

Hata hivyo, Wakenya hawajakuwa na lao katika makala ya 2023 ambapo Waethiopia Amane Beriso (2:24:23) na Gotytom Gebreslase (2:24:34) na Mmoroko Fatima Ezzahra Gardadi (2:25:17) wamenyakua nafasi tatu za kwanza, mtawalia.

Mzawa wa Kenya, Mwisraeli Lonah Salpeter ameridhika na nafasi ya nne kwa 2:25:38 naye Muethiopia Yalemzerf Yehualaw akafunga tano-bora (2:26:13).

Mkenya wa kwanza Rosemary Wanjiru amemaliza katika nafasi ya sita kwa 2:26:42 akifuatiwa na Selly Kaptich (2:27:09).

Wanjiru alikuwa amepigiwa upatu kuwania medali vilivyo, hasa baada ya kuingia mashindano haya akiwa ndiye ana muda bora katika marathon ya wanawake mwaka 2023 kufuatia ushindi wake wa Tokyo Marathon wa 2:16:28 mwezi Machi.

  • Tags

You can share this post!

Wawili washtakiwa kudandia meli iliyobeba mibuyu kuelekea...

Vita baridi Mlimani kati ya Rigathi na Ndindi Nyoro

T L