• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Kenya yakabiliwa na kibarua kigumu dhidi ya Misri kutafuta tiketi ya Kombe la Dunia la walemavu

Kenya yakabiliwa na kibarua kigumu dhidi ya Misri kutafuta tiketi ya Kombe la Dunia la walemavu

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Kenya ya walemavu ina kibarua kigumu kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022 baada ya kukutanishwa na Misri katika nusu-fainali ya Kombe la Afrika ya kuorodhesha nambari tano hadi nane jijini Dar es Salaam, Tanzania mnamo Desemba 2.

Vijana wa kocha Willis Odhiambo watajibwaga uwanjani bila wachezaji nyota Nicholus Keiyo na Albert Mwakenga wanaotumikia marufuku.

Walionyeshwa kadi nyekundu katika mechi za makundi dhidi ya Zanzibar na mabingwa wa dunia Angola.

Kenya, ambayo ilishiriki Kombe la Dunia mwaka 2014 na 2018 nchini Mexico, ilijipata ikiwania nafasi ya tano hadi nane baada ya kulemewa na Ghana 4-0 katika robo-fainali mnamo Desemba 1.

Misri ilipoteza dhidi ya Angola kwa njia ya penalti 3-2 baada ya muda wa kawaida kutamatika 1-1 Jumatano.

Mshindi kati ya Kenya na Misri atakutana katika fainali ya nambari tano dhidi ya mshindi kati ya Morocco na Cameroon kuamua nani atajiunga na timu nne za kwanza kuwakilisha Bara Afrika kwenye Kombe la Dunia jijini Istanbul nchini Uturuki mwezi Oktoba 2022.

“Hatujawahi kukutana na Misri. Hata hivyo, ni wakali. Matumaini yetu ni kuwa tutaweza kuwadhibiti. Hata hivyo, ni kibarua kigumu kwa sababu tutakosa huduma za wachezaji wawili muhimu. Keiyo na Mwakenga wanatumikia marufuku kwa kupata kadi nyekundu,” timu ya Kenya ilisema mapema Alhamisi.

Tanzania, Angola, Liberia na Ghana zilijikatia tiketi ya kuwa katika Kombe la Dunia 2022 baada ya kushinda michuano yao ya robo-fainali.

  • Tags

You can share this post!

Hasira orodha ya mwisho ya kuwania tuzo ya fasihi ya...

KPA imeajiri Wapwani kupita kiasi, yadai ripoti

T L