• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Kibarua kikali EPL ikirejea

Kibarua kikali EPL ikirejea

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) itarejea hapo kesho Jumamosi baada ya mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia huku Arsenal ikikabiliwa na mtihani mgumu dhidi ya Liverpool wa kudumisha rekodi ya kutopoteza michuano minane iliyopita.

Vijana wa kocha Mikel Arteta wako katika orodha ya timu zinazofanya vyema zaidi wakati huu baada ya kuzoa ushindi mara sita ikiwemo kubwaga Aston Villa 3-1, Leicester 2-0 na Watford 1-0 katika tatu zilizopita, na kutoka sare dhidi ya Brighton 0-0 na Crystal Palace 2-2.

Ni rekodi ndefu ya ushindi kushuhudiwa na timu yeyote msimu huu kwenye EPL.

Hata hivyo, wanabunduki hao wanazuru ugani Anfield ambamo hawajazoa ushindi ligini katika mechi nane zilizopita.

Wamepoteza michuano mitano iliyopita kwa jumla ya mabao 18-4.

Isitoshe, Liverpool hawajapigwa Anfield katika mechi tisa mfululizo ligini, ingawa walikabwa 2-2 na Manchester City na Brighton katika mbili zilizopita.

Vijana wa Arteta watakuwa mawindoni kutafuta ushindi wa kwanza ligini uwanjani Anfield tangu Septemba 2012 walipovuna 2-0 kupitia mabao ya wachezaji wa zamani Lukas Podolski na Santi Cazorla.

Mara ya mwisho, hata hivyo, Arsenal kupata ushindi Anfield ni mwaka mmoja uliopita kwenye kipute cha Carabao kwa njia ya penalti 5-4.

Macho yatakuwa kwa wavamizi matata Mohamed Salah (Liverpool) na Pierre-Emerick Aubameyang katika mchuano wa kesho.

Katika kipindi cha miezi miwili, Arsenal wameruka kutoka nafasi ya 20 (mwisho) hadi nambari tano. Wana alama 20, mbili nyuma ya Liverpool ya kocha Jurgen Klopp inayoshikilia nafasi ya nne.

Jumla ya mechi nane zitasakatwa Jumamosi ikiwemo inayokutanisha viongozi Chelsea dhidi ya Leicester inayotapatapa. Kocha Thomas Tuchel anatarajiwa kukaribisha mfumaji matata Romelu Lukaku kutoka mkekani dhidi ya Leicester.

You can share this post!

Kenya yaamua kusubiri Fifa itoe marufuku ya soka nchini

Rais afariji Tuju kwa kumpoteza mamake

T L