• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Kigogo Sami Khedira wa Ujerumani kuangika daluga zake za usogora mwisho wa msimu huu

Kigogo Sami Khedira wa Ujerumani kuangika daluga zake za usogora mwisho wa msimu huu

Na MASHIRIKA

KIUNGO Sami Khedira aliyekuwa sehemu ya kikosi kilichoshindia Ujerumani Kombe la Dunia mnamo 2014 nchini Brazil, atastaafu rasmi kwenye ulingo wa soka mwishoni mwa msimu huu baada ya waajiri wake Hertha Berlin kupepetana na Hoffenheim mnamo Mei 22, 2021.

Mchuano huo ndio utakuwa wa mwisho kwa Hertha Berlin kutandaza kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) msimu huu.

Maamuzi ya Khedira, 34, kuangika daluga zake kwenye ulingo wa soka yanafanyika miezi mitatu pekee baada ya sogora huyo kubanduka kambini mwa Juventus na kuingia katika sajili rasmi ya Hertha.

Akiwa Juventus, aliongoza miamba hao wa soka ya Italia kunyanyua mataji matano ya Ligi Kuu (Serie A).

Khedira atastaafu akijivunia kutwaa jumla ya mataji 16 katika kipindi cha miaka 14 ya usogora. Aliwahi kuongoza Real Madrid ya Uhispania kuzoa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) baada ya kushindia Stuttgart ufalme wa Bundesliga.

“Ni wakati wa kusema kwaheri. Imekuwa tija na fahari tele kuwania mataji katika vikosi mbalimbali na kujishindia baadhi. Kubwa zaidi ninalojivunia ni kuwa sehemu ya historia wakati Ujerumani walipotwaa Kombe la Dunia mnamo 2014,” akaandika Khedira kwenye mtandao wake wa Instagram.

Khedira aliwahi kuugua maradhi ya moyo mnamo Februari 2019 akichezea Juventus. Hata hivyo, alitibiwa na kupona na akarejea ulingoni ambapo alishindia Juventus mataji mawili katika soka ya Italia kabla ya kurejea Ujerumani kuvalia jezi za Hertha.

Khedira atastaafu wiki moja baada ya Hertha kuambulia sare tasa dhidi ya Cologne na kuponea chupuchupu kuteremshwa ngazi kwenye Bundesliga msimu huu. Sogora huyo amechezea Hertha mara nane kufikia sasa na huenda akawajibishwa dhidi ya Hoffenheim mnamo Mei 22, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Liverpool wapepeta Burnley na kuingia ndani ya mduara wa...

Mwanamume ajirusha kutoka orofa ya kumi Mombasa