• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:42 PM
Kinda Bukayo Saka hakustahili kupewa jukumu kubwa la aina hiyo – Roy Keane

Kinda Bukayo Saka hakustahili kupewa jukumu kubwa la aina hiyo – Roy Keane

Na MASHIRIKA

ALIYEKUWA nahodha wa Manchester United, Roy Keane, amelaumu Uingereza kwa kumpa Bukayo Saka jukumu la kupiga mkwaju wa penalti katika mechi yao dhidi ya Italia iliyowahakikishia ushinde katika uwanja wa Wembley jijini London.

Penalti ya Saka, 19, ilikuwa ya uamuzi muhimu ikiwa ya mwisho wakati Italia wakiongoza 3-2.

Lau angefunga, penalti za ziada zingepigwa ila ilipanguliwa na mlinda-lango wa Azzuri Gianluigi Donnarumma aliyekuwa amempangulia pia Jadon Sancho naye Rashford akiwa tayari alielekeza mpira kwa mlingoti wa goli.

Keane anashikilia kuwa wachezaji wenye tajriba ya muda mrefu katika soka walifaa kupiga mkwaju huo badala ya kinda huyo,

“Wachezaji kama Sterling ama Grealish hawafai kukaa na kumwachia kinda kama huyo kibarua hicho kigumu,” raia huyu wa Ireland aliambia ITV.

Meneja wa AS Roma, Jose Mourinho alisisitiza maneno ya Keane, akizungumza na talkSport. Alisema kuwa kuweka hatima ya taifa mikononi mwa kinda kama huyo ni hatua nzito kwa wakati huu.

“Sijui swali hili nimuulize kocha Southgate au vipi. Mara nyingi wachezaji hawa huepuka majukumu yao wanapohitajika,” alisema.

Kiungo wa Uingereza Jack Grealish alijitoa lawamani akieleza nia yake ya kupiga mkwaju wa penalti ambayo haikutimizwa.

“Siwezi kusukumiwa lawama kwa kutopiga penalti, hali niliomba kibali hicho. Msimamizi wetu amechukua hatua nzuri katika taji hili na usiku huu alifanya hivyo pia,” alisema Grealish kupitia mtandao wake wa Twitter.

Kulingana na aliyekuwa difenda wa Uingereza Garry Neville, mipango yote ya wale waliostahili kuwakilisha taifa mechi ikiishia kuamuliwa kwa penalti walifaa kuchaguliwa mapema; wakati wa maandalizi.

Hata hivyo, aliyekuwa difenda wa Uingereza Rio Ferdinard amesema haifai kuwaelekezea kidole cha lawama waliopoteza penalti. Alan Shearer naye amewasifu vijana waliojikakamua kukubali majukumu hayo ijapokuwa mazito.

“Kwa mchezaji kinda kukubali kupiga penalti, ni hatua kubwa inayofaa kusifiwa. Kwa sasa hali ni ngumu kwao, ila nawatakia afueni ya haraka,” alisema katika mahojiano na idhaa ya BBC.

TAFSIRI NA: NDUNGI MAINGI

You can share this post!

Kampuni yazindua kiwanda cha kuongeza thamani mazao mabichi...

Utalii, uwekezaji kuimarika Pwani – Wadau