• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Kipa aliyeanza kama difenda aisaidia KU Desert Roses kuzoa mataji

Kipa aliyeanza kama difenda aisaidia KU Desert Roses kuzoa mataji

Na PATRICK KILAVUKA

ALIANZA kucheza boli kama difenda.

Lakini alipojiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta, kocha wake alimpinda na kumgeuza kuwa kipa.

Mdakaji Naomi Jelagat Kemei, 23, amejitahidi kulinda lango la KU Desert Roses kwa udi na uvumba hadi kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi ya Vyuo Vikuu (KUSA) miaka minne kati ya mitano wametwaa mtawalia.

Mbali na Ligi ya Kanda ya Shirikisho la Soka Kenya msimu wa 2020-2021, Nairobi East (NERL) kabla kuteleza katika ngarambe ya kumpata bingwa wa Kanda ya Nairobi katika mashindano ambayo yaliandaliwa uga wa Ligi Ndogo ambapo alikubali magoli mawili kutoka kwa Uweza Queens ambao walikuwa mabingwa wa Ligi ya Nairobi West sawia na Kanda msimu huo.

Msimu mzima alikubali mabao matano. Alionyesha weledi wa kudaka mpira japo walishindwa kwani alidhibiti makombora ya wapinzani kama kipa shujaa.

Chini ya kocha Caroline Ajowi ambaye alimtambua tangu alipojiunga na Chuo cha Kenyatta (KU), anasema mnyakaji huyu ni yule aliye na ari ya kufanya mazoezi na kujituma kwani juhudi zake zimeipelekea timu kufika mbali katika mashindano.

“Anapenda kupiga shughuli ya boli kama kipa ambaye amejifunga nira ya kufia timu. Isitoshe, nidhamu na upangaji wa ngome yake humrahishia mambo mchumani,” asema kocha Ajowi ambaye amemlea mkamataji boli huyo aliye tokea Shule ya Upili ya Nakuru Girls High mwaka wa 2016.

Alikuwa amepata masomo ya msingi katika shule ya Tuiyobei, Nyahururu.

 

Kipa Naomi Jelagat Kemei akifanya mazoezi na wenzake katika kikosi cha KU Desert Roses kujiandaa kwa fainali za FKF, Gatuzi la Nairobi uwanjani Ligi Ndogo. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Anasomea masuala ya utafiti wa biolojia ya viumbehai.

Katika michezo za shule ya sekondari – KSSA, alifika kiwango cha kanda ya Bonde Ufa ambayo iliandaliwa Shule ya Wavulana ya Kapsabet.

Amekamatia boli timu ya chuo ya Desert Roses na kuiwezesha kuwa bingwa manne mtawalia akiwa langoni.

Mbali na kuwa kipa wa chuo, alisajiliwa na timu ya Baringo Starlets mwaka wa 2018.

Isitoshe, udakaji wake ulimezewa mate na timu ya Eldoret Falcons japo kwa sababu ya mbano wa masomo hakupata nafasi ya kuenda kufanya mazoezi hali ambayo ilisababisha yeye kutoendelea na mikakati ya kuichezea.

Akirejelea Ligi ya FKF, anasema timu ambayo ilimpa kizungumti ilikuwa Ruai Queens kwani walimsumbua na hakupata utulivu langoni.

Je, yeye hujimuduaje kusawazisha masomo na talanta ikitiliwa maanani kwamba taaluma anayosomea ni ile ambayo inahitaji umakinifu sana na utafiti wa kina? Jelagat anasema kibarua tu ni kujua jinsi ya kujipanga kwani yeye anazama masomoni wakati yupo darasa na hudhuria mihadhara yote na muda wake wa ziada ndio anautumia kufanya mazoezi ya timu na ya kibinafsi.

Timu ambayo anaihusudu ni Chelsea. Kipa anayemzuzua langoni ni mdakaji Mendy wa Chelsea kutokana na jinsi anavyookoa mipira, kupaa na kujituma kwake.

Changamoto ambayo hupata ni majeraha madogomadogo ingawa hafi moyo katika kutekeleza wajibu kama mlindalango.

Yeye hutumia mbinu ya mawasiliano akiwa langoni kama njia ya kufanya ngome kuwa imara na kusisimua ndiposa ikabili wakinzani wao.

Cha mno hamna lingine ila, anatoa ushauri kwa wale ambao ni wanachuo na wanaotumia talanta kwamba, yawapasa wawe na hekima ya kusawazisha masomo na talanta na watavuna jasho lao la kujizatiti.

  • Tags

You can share this post!

Kiini cha Raila kuogopa kuitwa ‘mradi’ wa Uhuru

Leads United wahifadhi taji la Westlands Youth Soccer...

T L