• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Kiini cha Raila kuogopa kuitwa ‘mradi’ wa Uhuru

Kiini cha Raila kuogopa kuitwa ‘mradi’ wa Uhuru

Na LEONARD ONYANGO

KINARA wa ODM Raila Odinga anakabiliwa na kibarua kigumu kujitenga na madai kwamba yeye ni ‘mradi’ wa Rais Uhuru Kenyatta.

Rais Kenyatta tayari ameonyesha dalili zote kwamba anaunga mkono Bw Odinga kumrithi baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022 – hatua ambayo imefanya wapinzani na wadadisi kuamini kwamba waziri mkuu huyo wa zamani ni mradi wa Ikulu.

Kulingana na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama cha Amani National Congress (ANC) Barrack Muluka, hatua ya Rais Kenyatta kumwalika Bw Odinga kuzungumza katikati ya hotuba yake wakati wa maadhimisho ya sherehe za Jamhuri, Jumapili iliyopita, ilikuwa ishara tosha kwamba kinara wa ODM ni mradi wake.

Anasema hatua ya Rais Kenyatta kumpa Bw Odinga fursa ya kuzungumza katikati ya hotuba yake ilikuwa sawa na kusema kwamba ‘Raila Tosha’.

AZMA YA URAIS

“Bw Odinga alipotangaza azma yake ya kuwania urais 2022 uwanjani Kasarani, hafla hiyo ilihudhuriwa na karibu mawaziri wote. Hiyo ni ishara tosha kwamba Raila ni mradi wa Rais Kenyatta,” anasema Dkt Muluka.

Anasema kuwa hatua ya mabwanyenye wa Mlima Kenya – ambao walisadia Rais Kenyatta kushinda urais 2013 na 2017 – kutangaza kwamba watampa Bw Odinga mwaniaji mwenza Februari 2022, pia ilikuwa ishara kuwa kinara wa ODM ni mradi wa Ikulu.

Mwakilishi wa Wanawake wa Uasin Gishu Gladys Boss anadai kuwa mkutano wa Azimio la Umoja uliofanyika Kasarani, ulifadhiliwa na serikali na mabwanyenye wa Wakfu wa Mlima Kenya (MKF).

HAKUNA UBAYA

Lakini, Dkt Muluka, hata hivyo, anasema kuwa hakuna ubaya kwa Rais Kenyatta kuwa na mwanasiasa ambaye ni mradi wake katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

“Viongozi wengi kote ulimwenguni wanapoondoka madarakani huwa na miradi yao. Hivyo, sioni ubaya wowote kwa Rais Kenyatta kuwa na mradi wake,” anasema.

Naibu wa Rais William Ruto pamoja na wandani wake wamekuwa wakisisitiza kuwa Bw Odinga ni mradi wa Rais Kenyatta.

Wadadisi wanasema kuwa hatua hiyo ya Naibu wa Rais inalenga kumnyima kura Bw Odinga katika maeneo ambapo Rais Kenyatta amepoteza ushawishi na umaarufu wa kisiasa.

Wakili na Mtaalamu wa Masuala ya Utawala, Javas Bigambo anasema kuwa iwapo Bw Odinga atakiri kuwa mradi wa Rais Kenyatta atapoteza kura nyingi katika maeneo ya Mlima Kenya ambapo umaarufu wa serikali ya Jubilee umedidimia.

Wanasiasa wa Mlima Kenya wamekuwa wakigura Jubilee na kujiunga na chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Dkt Ruto.

Baadhi ya wanasiasa wa Mlima Kenya ambao hawajajiunga na UDA, wameanza harakati za kugura Jubilee na kujiunga na vyama vidogo kwa lengo la kutetea viti vyao.

Bw Bigambo anasema kuwa kura za Bw Odinga hazitapungua katika maeneo yanayochukuliwa kuwa ngome yake kama vile Nairobi, Nyanza, Pwani na Magharibi hata akikiri kuwa mradi wa Rais Kenyatta.

Washauri wa Bw Odinga, hata hivyo, wanahofia kuwa kinara wa ODM kubandikwa jina la ‘mradi wa Uhuru’ ni hatari kwani anaweza kukataliwa na wapigakura wakidhani ataendeleza ‘mabaya’ ya serikali ya Jubilee.

Wanahofia matokeo ya 2002 ambapo Uhuru Kenyatta aliungwa mkono na Rais Daniel arap Moi na kuwaacha wanasiasa waliobobea kama vile Bw Odinga ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Kanu wakati huo.

Uhuru alibandikwa jina la ‘Mradi wa Moi’ na hatimaye alibwagwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

Aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khawale anasema kuwa Bw Odinga atakataliwa na Wakenya iwapo Wakenya watabaini kuwa ni mradi wa Rais Kenyatta.

“Mnamo 2002 Moi alijaribu kulazimishia Wakenya ‘Mradi Uhuru’ akafeli. Miaka 20 baadaye, Rais Kenyatta analazimishia Wakenya ‘Mradi Raila’ ataanguka,” anasema.

Wadadisi wanasema kuwa Uhuru alishindwa 2002 kwa sababu Wakenya walihitaji mabadiliko na walikuwa wamechoshwa na serikali ya Kanu.

“Serikali ya Jubilee imekuwa ikisutwa kwa mabaya mengi kama vile kupanda kwa gharama ya maisha, kukita mizizi kwa ufisadi, kushindwa kusaidia mamilioni ya vijana kupata ajira, mzigo wa deni la kitaifa, ukaidi wa maagizo ya mahakama kati ya maovu mengineyo mengi. Raila akikubali kuitwa ‘mradi wa Uhuru’ kuna hatari ya kukataliwa na Wakenya kwani watadhani ataingia mamlakani kuendeleza mabaya hayo ya serikali ya Jubilee na kulinda mali ya mabwanyenye,” anasema Wakili Felix Otieno.

You can share this post!

Ngilu: Mwanasiasa wa kike mwenye ujasiri wa aina yake

Kipa aliyeanza kama difenda aisaidia KU Desert Roses kuzoa...

T L