• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Kipa Opiyo akubali mkataba mpya kuchezea Ingwe

Kipa Opiyo akubali mkataba mpya kuchezea Ingwe

NA JOHN ASHIHUNDU

HATIMAYE kipa Levis Opiyo amekubali kuendelea kuchezea AFC Leopards baada ya mlinda lango huyo kukubali mkataba mpya wa miaka miwili.

Opiyo aliyejiunga na Ingwe mnamo Novemba 2021 amekuwa kipa chaguo la kwanza, akisaidiwa na chipukizi Maxwell Mulili ambaye pia amekubali kandarasi ya miaka mitatu.

Wengine ni pamoja na Cliff Nyakeya zamani staa wa Wazito FC ambaye amesaini mkataba mpya wa mwaka mmoja kuendelea kusakatia Ingwe baada ya kujiunga na mabingwa hao wa zamani mwezi Januari.

Nahodha wa timu hiyo, Eugene Mukangula pia amekubali kubakia kikosini pamoja na mlinzi matata Tedian Esilaba, mshambuliaji matata Ojo Olaniyi Fasanmi, kutoka taifa la Nigeria.

Nyakeya ambaye awali aliwahi kuchezea Masri ya Misri baada ya awali kusakatia timu za Gor Mahia na Mathare United alisema anajawa na furaha tele baada ya Ingwe kumpa mkataba mpya.

Kadhalika Leopards imefanikiwa kuwabakisha kikosini Jaffari Odeny Owiti mwenye umri wa miaka 24, beki mzoefu Collins Shivachi, Robert Mudenyu, kipa chipukizi Maxwell Mulili pamoja na kiungo mshambuliaji Mousa Saad, raia wa Sudan Kusini.

Wakati huo huo, kocha Patrick Aussems wa AFC Leopards atarejea nchini Agosti 24 baada ya kukosa kutua mwishoni mwa wiki kutokana na heka heka za uchaguzi mkuu zinazoendelea nchini.

Akitoa habari hiyo, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Gilbert Andugu amesema kocha huyo amekuwa nchini Ubelgiji kwa likizo, lakini anatarajiwa kurejea Nairobi mwishoni mwa wiki kuendelea kukinoa kikosi hicho kabla ya msimu mpya kuanza Septemba 10.

Licha ya kurejea kwake kusukumwa mbele, Andugu amesisitiza kwamba kocha huyo mwenye umri wa miaka 59 atarejea nchini Agosti 24 kuendelea kutekeleza jukumu lake, baada ya hapo awali kukubali mkataba mpya wa miaka miwili.

“Ningependa kuwahakikishia mashabiki kwamba kocha wetu haendi popote, licha ya madai yanayovumishwa na baadhi ya vyombo vya habari,” alisema Andugu.

“Tulichunguza jinsi hali ilivyo nchini kwa sasa tukaamua angojee hadi hali itakapotulia. Amekuwa akiwasiliana na masaidizi wake wa kamati ya kiufundi,”

Andugu alisema huku akiongeza kwamba klabu inafanya kila iwezalo kuhakikisha wachezaji wote muhimu wamebakia kwenye klabu hiyo kwa ajili ya msimu ujao.

“Tunahitaji wachezaji wote waliosaidia timu kumaliza katika nafasi ya tano msimu uliopita, wakati huu tunalenga kutwaa ubingwa baada ya kusubiri tangu 1998,” aliongeza Andugu.

Aussems amekuwa likizoni barani Ulaya tangu msimu uliomalizika uishe, huku mashabiki wa klabu hiyo wakipagia katika hali ya kutojua iwapo atarejea nchini kuendelea kunoa klabu yao.

  • Tags

You can share this post!

Ruto awataka machifu waliotekwa na wanasiasa warejee kazini

Ruto asema mawaziri katika serikali yake watawajibishwa...

T L