• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 AM
Kipaji cha beki huyu chaimarika kadri anavyojituma

Kipaji cha beki huyu chaimarika kadri anavyojituma

Na PATRICK KILAVUKA

MJA anapoichochea talanta, huanza kuona ikijitokeza na kukita mizizi hatua kwa hatua.

Hali hii ni sawa na ya mwanasoka John Kamau ambaye anasema licha kwamba aliamini kuwa na kipawa cha kabumbu ndani mwake, kubanwa na wazazi kushiriki mchezo huo kwa kumhimizwa azingatie masomo kuliko kusakata kandanda kuipelekea talanta yake kulala kiporo akiwa shule ya msingi japo ilianza kupata mashiko akiwa shule ya upili.

“Nikiwa shule ya msingi, sikucheza mpira wa ushindani. Ila, nilikuwa tu ninacheza na watoto wengine kwenye ploti tukipiga boli ambayo tuliunda kutokana na nyuzi za manila na makaratasi. Isitoshe, singeruhusiwa kucheza kwa sababu wazazi wangu walinihimiza kuyapa masomo kipaumbele, ” akiri Kamau ambaye alipata masomo ya msingi Shule ya New Kihumbuini kabla kujiunga na Shule ya Upili ya Anadamaga, Kangemi, Kaunti ya Nairobi.

Difenda Kamau aliweza kukumbatia soka akiwa shule ya sekondari hadi akapiga soka daraja ya kaunti ndogo ya Westlands katika Chama cha Michezo ya Shule za Upili (KSSSA).

Kabla kujiunga na timu ya mtaani ya Red Carpet ambayo amedumu nayo kwa miaka minane, aliichezea Muthangari Academy kwa mwaka mmoja.

Ameikumbatia timu ya Carpet hadi wakati huu ambapo wanacheza Ligi ya Kanda ya FKF, Nairobi West.

Akiwa kikosini mwa Carpet, anajivunia kukisaidia kubeba taji la kipute cha makala ya sita mwaka cha Tim Wanyonyi Super Cup, 2018 baada ya kufyeka Leads United penaliti 5-4 baada ya sare ya 1-1.

Mwanadimba huyu anakiri kwamba,mikononi mwa kocha wa Carpet Meshack Onchonga ameweza kuchongwa ubutu wa kipawa chake hadi amedhibiti safu yake na kuisaidia timu katika ligini.

“Yeye huniambia nisikate tamaa na nisichoke kujituma kwa kuwa bahati ya mtu hailaliwi mlango wazi na siku moja nitapata matunda ya jasho langu licha ya changamoto kuwepo,” anakariri mwanasoka huyo ambaye husaka riziki huku akijitahidi kusakata boli kwani ari na matamanio yake ni kufika upeo wa kipaji chake majaliwa na Mualana.

Anasema changamoto kuu kwake ni kusawazisha muda wa kufanya kazi na mazoezi.

Mwanakabumbu huyu ni shabiki wa timu ya Arsenal ambako mchezaji anamhusudu Pierre- Emerick Aubameyany anapiga soka.

Anadokeza kwamba mchezo aliowahi kuufurahi ni mwaka 2018 ambapo kuandaliwa fainali za Kombe la Dunia nchini Russia na France na ikaipepeta Croatia 4-2 na kutwaa taji japo kwa jasho.

Milango ya heri ya kuchezea timu za kitaifa ikifunguka, angependa kusakatia soka timu ya Gor Mahia na Harambee Stars kwani anaamini ustahamilivu ni muhimu kwa mja kufaulu maishani.

  • Tags

You can share this post!

Mhasibu ashtakiwa kwa kuvuruga mfumo wa malipo wa shirika...

CARABAO CUP: Arsenal walazimishia Liverpool sare tasa...

T L