• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Kisumu All Stars, Zoo Kericho ugani wikendi

Kisumu All Stars, Zoo Kericho ugani wikendi

Na CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa Kisumu All Stars Salim Babu amesema kuwa timu hiyo inalenga ushindi wake wa kwanza msimu huu katika mechi ya wikendi dhidi ya viongozi wa Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) AP Bomet ugani Silibwet.

Mechi hiyo itakuwa kati ya nyingine nane ambazo zimeratibiwa zitasakatwa Jumamosi na nyingine nne mnamo Jumapili ligi hiyo ikiingia raundi ya tano baada ya kurejelewa wiki jana.Kisumu All Stars ambayo ipo kwenye msimu wake wa pili katika ligi hiyo baada ya kushushwa ngazi kutoka NSL misimu miwili iliyopita, imekuwa ikipata matokeo duni na bado haijaonja ushindi wowote.

Timu hiyo iliagana sare ya 1-1 dhidi ya Zoo Kericho mnamo Novemba 6, Ikalemewa 2-1 na Modern Coast mnamo Novemba 13 kabla ya kuangushwa 1-0 na Naivas wikendi iliyopita.Hata hivyo, Babu anasema tatizo lao limekuwa la ufungaji wa mabao baada ya baadhi ya waliokuwa wachezaji wao msimu uliopita kuhama na kujiunga na timu nyingine za ligi kuu.

“Wachezaji wetu saba walisajiliwa na timu nyingine hasa zile zinazoshiriki ligi kuu. Kujaza hilo pengo limekuwa mtihani kwetu ila wachezaji wangu katika kikosi cha sasa nao wamekuwa wakitia bidii. Naamini tutapata ushindi wetu wa kwanza kesho japo AP Bomet pia ni timu kali,” akasema Babu.

AP Bomet inaongoza ligi hiyo kwa alama 12 kwa kuwa ndiyo timu pekee ambayo imeshinda mechi zake zote nne hadi sasa. Pia timu hiyo inayolenga kupanda hadi ligi kuu haijafungwa bao lolote.Kando na Kisumu All Stars, Zoo Kericho ambayo ilishiriki Ligi Kuu msimu uliopita pia ni timu nyingine ambayo imekuwa ikifanya vibaya kwenye NSL.

Timu hiyo pia haijaonja ushindi, huku ikisajili sare mara mbili na kupoteza katika michuano miwili.Hata hivyo, Kocha wa Zoo Kericho Herman Iswekha anasema bado ni mapema kutabiri kuwa hawatafanya vizuri msimu huu kutokana na matokeo hayo.

Kama tu Babu, Iswekha pia anapania ushindi watakapochuana na Mwatate United ugani Wundanyi hapo kesho.“Vijana wangu bado hawajapata makali yao ila nimewatazama kwa makini na wamekuwa wakiimarika sana. Tunaenda Wundanyi kupigania ushindi wetu wa kwanza ili kuwapa vijana wangu motisha kwenye mechi zinazokuja,” akasema Iswekha.

You can share this post!

KEFWA kuandalia nyota kutoka Ligi Kuu ya wanawake tuzo ya...

Dereva Varese kutifua vumbi Guru Nanak Rally

T L