• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Kiungo Jorginho wa Chelsea atawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Uefa

Kiungo Jorginho wa Chelsea atawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Uefa

Na MASHIRIKA

KIUNGO matata wa Chelsea na timu ya taifa ya Italia, Jorginho Luiz Frello, 29, ametawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa 2020-21 na Shirikisho la Soka la Bara Ulaya (Uefa).

Nyota huyo aliwapiku wanasoka N’Golo Kante wa Chelsea na Kevin de Bruyne wa Manchester City katika vita vya kuwania tuzo hizo.

Thomas Tuchel alitia kibindoni tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka baada ya kuongoza Chelsea kunyanyua taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2020-21.

Nahodha wa Barcelona, Alexia Putellas ndiye aliyetawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka kwa upande wa wanawake.

Jorginho alicheza jumla ya mechi 56 katika ngazi ya klabu na timu ya taifa msimu uliopita na akafunga mabao tisa. Alivunia Chelsea ufalme wa UEFA na kuongoza Italia kupepeta Uingereza na kutia kapuni ubingwa wa Euro.

Sogora huyo alianza kampeni za msimu huu wa 2021-22 kwa kuongoza Chelsea kutwaa taji la tatu la Uefa, Super Cup baada ya kupepeta Villarreal ya Uhispania jijini Belfast, Ireland Kaskazini.

Mlinda-lango wa Chelsea, Edouard Mendy aliibuka Kipa Bora wa Mwaka baada ya kutofungwa katika mechi tisa za UEFA. Kante ambaye ni raia wa Ufaransa alituzwa taji la Kiungo Bora wa Mwaka.

Tuzo ya Beki Bora wa Mwaka ilimwendea Ruben Dias ambaye katika msimu wake wa kwanza ugani Etihad, alisaidia Man-City kutinga fainali ya UEFA kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.

Tuchel aliongoza ufufuo wa makali ya Chelsea kuanzia Januari 2021 baada ya kuaminiwa kuwa mrithi wa Frank Lampard aliyetimuliwa kwa sababu ya matokeo duni. Chini ya kipindi cha miezi minne, mkufunzi huyo raia wa Ujerumani alisaidia waajiri wake kupepeta Man-City 1-0 kwenye fainali ya UEFA jijini Porto, Ureno.

Erling Braut Haaland, 21, wa Borussia Dortmund alitawazwa Mshambuliaji Bora wa Mwaka.

Simon Kjaer ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Denmark na kikosi cha matabibu kilichookoa maisha ya kiungo Christian Eriksen aliyeanguka ghafla na kuzimia uwanjani wakati wa mechi ya Euro katika ya Denmark na Finland, walituzwa taji la Rais wa Uefa, Aleksander Ceferin.

Barcelona walitamalaki tuzo za upande wa wanawake kwa kujizolea mataji yote isipokuwa moja.

Zaidi ya kutawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka, nahodha Alexia Putellas pia alinyakua tuzo ya Kiungo Bora wa Mwaka.

Wenzake Sandra Panos na Jennifer Hermoso walitawazwa Kipa Bora na Beki Bora wa Mwaka mtawalia.

Lluis Cortes alitawazwa Kocha Bora wa Mwaka baada ya kuongoza Barcelona kunyanyua taji la Ligi Kuu (Primeria Division) na kuongoza waajiri wake kunyakua taji la kwanza la UEFA baada ya kuzamisha Chelsea jijini Gothenburg, Uswidi.

Irene Paredes wa Paris St-Germain (PSG) alitawazwa Beki Bora wa Mwaka na hivyo kunyima Barcelona mataji yote katika kategoria ya tuzo za wanawake.

TUZO ZA UEFA (Wanaume):

Mchezaji Bora wa Mwaka – Jorginho (Chelsea)

Kocha Bora wa Mwaka – Thomas Tuchel (Chelsea)

Kipa Bora wa Mwaka – Edouard Mendy (Chelsea)

Beki Bora wa Mwaka – Ruben Dias (Manchester City)

Kiungo Bora wa Mwaka – N’Golo Kante (Chelsea)

Fowadi Bora wa Mwaka – Erling Braut Haaland (Borussia Dortmund)

Tuzo ya Rais wa Uefa – Nahodha wa Denmark, Simon Kjaer na kikosi cha madaktari

(Wanawake):

Mchezaji Bora wa Mwaka – Alexia Putellas (Barcelona)

Kocha Bora wa Mwaka – Lluis Cortes (Barcelona)

Kipa Bora wa Mwaka – Sandra Panos (Barcelona)

Beki Bora wa Mwaka – Irene Paredes (PSG)

Kiungo Bora wa Mwaka – Alexia Putellas (Barcelona)

Fowadi Bora wa Mwaka – Jennifer Hermoso (Barcelona)

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Askofu akubali kumtunza mtoto wa kambo

Wandani wa Rais Mlimani watumia BBI kuponda Ruto