• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 7:55 PM
Wandani wa Rais Mlimani watumia BBI kuponda Ruto

Wandani wa Rais Mlimani watumia BBI kuponda Ruto

Na JUSTUS OCHIENG

WANDANI wa Rais Uhuru Kenyatta wameanzisha kampeni ya kutumia mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) uliotupiliwa mbali na mahakama kupunguza ushawishi wa Naibu wa Rais William Ruto katika eneo la Mlima Kenya.

Washirika wa Rais Kenyatta sasa wanadai kuwa hatua ya Dkt Ruto kusherehekea baada ya mahakama kutupilia mbali mpango wa BBI ni ithibati kwamba hatakii mema eneo la Mlima Kenya.

Wakizungumza katika hafla mbalimbali, viongozi wa Mlima Kenya, walisema mpango wa Dkt Ruto ni kujifaidi mwenyewe badala ya kutetea haki za wakazi wa eneo la Mlima Kenya.

Walisema kuwa badala ya Dkt Ruto kuwaunga mkono rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odiga, yeye aliwashutumu na kuwaambia waangazie mahitaji ya Wakenya badala ya BBI.

Wandani hao wamesema kuwa kufutiliwa mbali kwa BBI na mahakama kutaathiri eneo la Mlima Kenya hasa kutokana na uwakilishi mbaya bungeni.

Mbunge wa Nyeri Mjini, Bw Wambugu Ngunjiri, alimshutumu Dkt Ruto huku akisema kuwa anashindwa ni kwa nini hatakii mema eneo la Mlima Kenya.

“Alikataa kutuunga mkono katika mjadala wa ugavi wa rasilimali za Kitaifa. Alipinga mchakato wa BBI ambao ungetatua suala la ugavi wa rasilimali za kitaifa, uwakilishi sawa, uwepo thabiti wa ukanda katika uongozi wa kitaifa na ulinzi wa majimbo ya Mlima Kenya yaliyo hatarini,” akasema Bw Ngunjiri mnamo Alhamisi.

Kulingana na mchakato huo wa BBI, serikali za Kaunti zingekuwa na ongezeko la sehemu ya mapato kutoka asilimia 16.9 hadi asilimia 35 ya mapato yote yaliyokusanywa.

Mbunge maalum wa Jubilee, Maina Kamanda, alisema kuwa eneo la Mlima Kenya limekuwa likikumbwa na tatizo la uchache wa maeneo bunge.

Mchakato wa BBI ulipendekeza ongezeko la idadi ya maeneo bunge 70, hatua ambayo ingesaidia eneo la Mlima Kenya kunufaika zaidi.

Kaunti ya Kiambu ingepata idadi kubwa ya maeneo bunge katika eneo la Mlima Kenya huku kaunti za Nakuru(3), Meru (2), Embu, Kirinyaga, Murang’a na Laikipia zikinufaika kwa eneo moja kila moja.

“Waliopata hasara zaidi kutokana na kutupiliwa mbali kwa BBI ni eneo la Mlima Kenya na yeyote anayesherehekea ni adui wetu,” akasema Bw Kamanda, Alhamisi.

Akiongezea, alisema kuwa juhudi za Rais kujaribu kutetea eneo hilo zitasalia kuwa kumbukumbu.

“Eneo la Mlima Kenya limepoteza nafasi ya uwakilishi sawa,” akaongeza Bw Kamanda.

Kwa upande wake, Gavana wa Kaunti ya Kirinyaga, Bi Ann Waiguru alisema eneo la Mlima Kenya linapanga kuungana ili kuangazia namna ya kuendelea mbele.

“Tunahitaji kuweka watu wetu pamoja ili tuweze kuzungumza kwa sauti moja,” akasema Bi Waiguru.

Aliyekuwa waziri wa kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri ambaye hamuungi mkono Dkt Ruto, alisema eneo hilo litampigia debe rais atakayetatua suala la uwakilishi eneo la Mlima Kenya.

“Mchakato wa BBI ambao tulitarajia ungeleta mabadiliko eneo la Mlima Kenya umetupiliwa mbali. Tunataka rais tutakayemchagua ahakikishe kuwa katika siku 100 zake mamlakani, atashughulikia suala la uwakilishi ama kupitia kura ya maoni au ukaguzi wa mipaka,” akasema Bw Kiunjuri.

You can share this post!

Kiungo Jorginho wa Chelsea atawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka...

Serikali yajipanga kuchanja mamilioni