• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:50 AM
Kiungo Matt Ritchie aomba msamaha kwa kumchemkia kocha wake Steve Bruce mazoezini

Kiungo Matt Ritchie aomba msamaha kwa kumchemkia kocha wake Steve Bruce mazoezini

Na MASHIRIKA

KIUNGO Matt Ritchie wa Newcastle United amewaomba mashabiki msamaha na kutaka kocha na kikosi chote kumwia radhi kwa kosa la kumchemkia kocha wake Steve Bruce wakiwa mazoezini.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 alimzomea Bruce mazoezini wiki hii baada uhusiano wao kuonekana kuvurugika mnamo Februari 27 mwishoni mwa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyoshuhudia Newcastle wakilazimishiwa sare ya 1-1 na Wolves.

Ritchie alikerwa na matamshi ya kocha wake baada ya mechi hiyo ambapo Bruce alisema mchezaji huyo hakuzingatia maagizo aliyompa wala kuwasilishia wenzake aliokuwa amempa kabla ya kuingia ugani katika kipindi cha pili cha mchezo.

Dakika chache baada ya Ritchie kuingia uwanjani, Newcastle walifungwa na Wolves, jambo ambalo Bruce alisema lisingetokea iwapo maagizo yake yangewasilishwa kwa wanasoka wengine jinsi alivyokusudia.

Mbali na Ritchie, wachezaji wengine waliosutwa na kocha Bruce baada ya mechi dhidi ya Wolves ni kipa Martin Dubravka, beki Jamal Lewis na fowadi Joelinton Cassio.

Baada ya kushinda mechi mbili pekee kutokana na 15 zilizopita, Newcastle kwa sasa wananing’inia padogo jedwalini kwa alama 26, nane nyuma ya Wolves ambao wana pointi sawa na Crystal Palace.

Newcastle kwa sasa wanajiandaa kuvaana na West Brom ambao kwa pamoja na Fulham na Sheffield United, pia wapo katika hatari ya kuteremshwa ngazi mwishoni mwa msimu huu. Pigo kubwa kwa Bruce katika mechi hiyo ni ulazima wa kukosa huduma za wanasoka Callum Wilson, Miguel Almiron na Allan Saint-Maximin wanaouguza majeraha. Watatu hao wamefunga jumla ya mabao 16 kati ya 27 ya Newcastle kufikia sasa msimu huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Chelsea yafunza Liverpool kusakata soka ya EPL

Bandari iko tayari kulima Nzoia Sugar