• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Chelsea yafunza Liverpool kusakata soka ya EPL

Chelsea yafunza Liverpool kusakata soka ya EPL

Na MASHIRIKA

BEKI Andy Robertson amewataka wenzake wa Liverpool kutopotezewa dira na mafanikio ya msimu uliopita na kuamakinikia kampeni za muhula huu wa 2020-21 na kucheza ipasavyo kama mabingwa watetezi.

Hii ni baada ya kikosi hicho cha kocha Jurgen Klopp kupokezwa kichapo cha tano mfululizo ligini katika uwanja wao wa nyumbani kwa mara ya kwanza baada ya kupigwa 1-0 na Chelsea mnamo Alhamisi ugani Anfield.

Mechi zote tatu za EPL zilizosakatwa Alhamisi zilishuhudia vikosi vilivyokuwa vikichezea nyumbani vikipokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa wageni. West Brom walipigwa 1-0 na Everton uwanjani The Hawthorns huku Tottenham Hostpur wakisajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Fulham ugani Craven Cottage.

Bao la Chelsea katika gozi dhidi ya Liverpool lilifumwa wavuni na fowadi chipukizi Mason Mount dakika tatu kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha kwanza kupulizwa.

Kichapo kikiwasaza Liverpool sasa katika vita vya kujinyanyua na kupigania fursa ya kumaliza kampeni ndani ya orodha ya timu nne za kwanza na hatimaye kufuzu kwa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Kwa upande wao, Chelsea kwa sasa hawajapoteza mechi yoyote kati ya 10 zilizopita chini ya kocha Thomas Tuchel aliyeaminiwa kuwa mrithi wa Frank Lampard aliyetimuliwa mnamo Januari 2021 kwa sababu ya matokeo duni.

Ushindi dhidi ya Liverpool uliwapaisha Chelsea hadi nafasi ya nne jedwalini kwa alama 47, nne zaidi kuliko Liverpool ambao kwa sasa wako katika hatari ya kupitwa na Tottenham Hotspur, Aston Villa na Arsenal katika vita vya kufukuzia nafasi za kunogesha soka ya bara Ulaya msimu ujao.

 Liverpool waliotwaa ubingwa wa EPL katika msimu wa 2019-20 wakijivunia pengo la alama 18 kati yao na kikosi kilichoambulia nafasi ya pili, hawakuwa wameshindwa katika mechi 68 za EPL nyumbani walipovaana na Burnley mnamo Januari 2021.

Tangu wakati huo, Liverpool wamepigwa na Brighton, Manchester City, Everton na Chelsea katika uwanja wao wa nyumbani wa Anfield.

“Msimu wa 2019-20 ulitamatika zamani na tukaanza mwingine. Licha ya kwamba sisi ni mabingwa watetezi wa taji la EPL, hatuchezi jinsi inavyostahili na tunazidi kushuka jedwalini kila kuchao,” akasema Robertson.

Ushindi huo pia wa Chelsea ulimvunia kocha Tuchel tija na fahari kubwa ikizingatiwa kwamba ilikuwa mara yake ya kwanza tangu 2009 kuongoza kikosi anachokinoa kushinda timu inayotiwa makali na Klopp.

Akidhibiti mikoba ya Borussia Dortmund ambayo pia iliwahi kujivunia huduma Klopp, Tuchel alishuhudia kikosi chake kikibanduliwa na Chelsea kwenye robo-fainali za UEFA kabla ya hali sawa na hiyo kushuhudiwa ugani Anfield alipokuwa akidhibiti pia mikoba ya PSG ya Ufaransa.

Liverpool watakuwa wenyeji wa Fulham katika mechi yao ijayo mnamo Machi 7 huku Chelsea wakipepetana na Everton ugani Stamford Bridge siku moja baadaye.

Kusuasua kwa Liverpool kumemfanya nahodha wao wa zamani, Graeme Souness, kukiri kwamba kikosi hicho kwa sasa kimeisha makali kabisa na kila timu inachangamkia fursa ya kukutana nayo kwa nia ya kuibwaga licha ya kwamba ndio mabingwa watetezi wa EPL.

“Matokeo ya Liverpool kwa sasa yanasikitisha na hawachezi kama mabingwa watetezi au timu iliyo na ari ya kushinda mechi. Sasa kila timu inataka fursa ya kucheza na Liverpool kwa kuwa wanaona ni wanyonge. Hilo ni jambo linaloumiza sana sisi mashabiki,” akasema Souness.

“Hali si shwari na hivyo ndivyo mambo yalivyo. Tulifungwa bao lililovuruga mpango wetu. Zimesalia mechi 12 pekee na pengo kati yetu na viongozi linazidi kuongezeka. Uthabiti wetu umeshuka na kiini cha hilo ni wingi wa majeraha ambayo yametulemaza kwenye safu ya ulinzi,” akasema Klopp kwa upande wake.

Liverpool  tayari wanakosa huduma za mabeki Virgil van Dijk, Joel Matip, Joe Gomez na kiungo Jordan Henderson.

MATOKEO YA EPL (Machi 4):

Fulham 0-1 Tottenham

West Brom 0-1 Everton

Liverpool 0-1 Chelsea

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Everton waambiwa na kocha wao waanze kujiandaa kwa soka ya...

Kiungo Matt Ritchie aomba msamaha kwa kumchemkia kocha wake...