• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Hatimaye mwafaka wapatikana Sudan

Hatimaye mwafaka wapatikana Sudan

KHARTOUM, Sudan

Na MASHIRIKA

UTAWALA wa jeshi nchini Sudan umekubali kumrejesha mamlakani Waziri Mkuu aliyeng’olewa mamlakani, Abdalla Hamdock, ambaye amekuwa akizuiliwa nyumbani kwake tangu mwezi uliopita.

Hili ni kulingana na mwafaka mpya ambao umefikiwa kati ya utawala huo, viongozi wa raia na makundi ya zamani ya wapiganaji.Hamdok aling’olewa mamlakani mwezi uliopita kufuatia mapinduzi ya kijeshi.

Mwafaka huo ulifikiwa kutokana na juhudi ambazo zimekuwa zikiendeshwa kuzipatanisha pande zote zinazozozana.Mnamo Oktoba 25, jeshi la taifa hilo lilitangaza hali ya hatari na kufutilia mbali serikali ya kiraia.

Mwafaka huo ulifikiwa Jumamosi usiku na kutiwa saini jana, kulingana na kiongozi wa Chama cha Umma, Fadlallah Nasir.“Mwafaka wa kisiasa umefikiwa kati ya Jenerali Burhan, Abdalla Hamdock, makundi ya kisiasa na mashirika ya kutetea haki za umma kumruhusu Hamdok kurejea katika nafasi yake.

Imefikiwa pia wafungwa wote wa kisiasa wataachiliwa huru,” akasema Nasir.Duru zilisema Hamdock amekubali masharti ya mwafaka huo kama njia ya kumaliza umwagikaji damu ambao umekuwa ukiendelea nchini humo.

Kundi la wapatanishi lilijumuisha wasomi, wanahabari na wanasiasa.Kundi hilo lilitoa taarifa ya kina inayoelezea masharti ya makubaliano hayo.Kando na kurejeshwa mamlakani kwa kiongozi huyo, utawala huo umekubali kuwaachilia huru maafisa wote wakuu wa serikali hiyo waliokuwa wamekamatwa.

Wapatanishi wanasema hilo ndilo litakuwa hatua ya kwanza kwa hali ya amani kurejea katika nchi hiyo.Jeshi la Sudan limekuwa kwenye mkataba wa kugawana mamlaka na vuguvugu la Forces for Freedom and Change (FCC) tangu Agosti 2019, baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo kwa muda mrefu, Omar el Bashir, kupinduliwa.

Vuguguvu hilo ni muungano wa mashirika kadhaa ya kutetea haki za binadamu.Sudan ilijipata kwenye mgogoro wa kisiasa mwezi uliopita, baada ya kiongozi wa jeshi, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kuvunja mrengo wa serikali ya raia na kuwakamata viongozi wake.

Alikuwa amepangiwa kung’atuka kama mwenyekiti wa Baraza Kuu la Utawala (SC) mwezi huu, ili kutoa nafasi kwa mwakilishi maalum wa FCC kuchukua uongozi wake.Katika kujitetea kwake, Burhan amekuwa akisisitiza kitendo cha jeshi hakikuwa “mapinduzi, bali juhudi za kuzima mapigano yaliyokuwa karibu kuibuka.”

Alisema makundi mbalimbali ya kisiasa yalikuwa yakiwachochea raia dhidi ya vikosi vya usalama.Baada ya mapinduzi hayo, alijitangaza kama kiongozi wa baraza jipya la utawala, huku akipata uungwaji mkono kutoka kwa jeshi na viongozi wa zamani wa makundi ya waasi.

Maelfu ya raia walifanya maandamano makubwa jijini Khartoum na miji mingine mikuu kulalamikia na kupinga mapinduzi hayo.Kwenye maandamano hayo, walichoma magurudumu huku wakiukashifu vikali utawala wa kijeshi kwa “kuhujumu mchakato wa kurejesha demokrasia nchini humo.”

Wanajeshi walijibu kwa kuwafyatulia risasi waandamanaji hao ili kuwatawanya.Kulingana na mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu, zaidi ya watu 40 wameuawa tangu makabiliano hayo kuanza.

Licha ya hatua hizo, mrengo mmoja wa FCC umekataa kutambua mkataba huo mpya. Badala yake, mrengo huo umepa kuendelea na mikutano mikubwa kuupinga.Jamii ya kimataifa ilikashifu vikali mapinduzi hayo, huku ikiutaka utawala huo kuwaachilia wafungwa wote wa kisiasa.

Kama ‘adhabu’ kwa utawala huo, Benki ya Dunia ilisimamisha misaada yote ya kifedha huku Umoja wa Afrika (AU) ukiiondoa nchi hiyo kama mwanachama wake kwa muda usiojulikana.

You can share this post!

Kocha auchemkia uongozi wa Ingwe Leopards kuhusu mishahara

Tundo ndiye mfalme wa KCB Thika Rally

T L