• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Kocha Beldine Odemba kutaja kikosi cha Harambee Starlets

Kocha Beldine Odemba kutaja kikosi cha Harambee Starlets

NA TOTO AREGE

KOCHA mpya wa Harambee Starlets Beldine Odemba, ametwikwa majukumu ya kuiongoza Starlets kwa mechi mbili za kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2024.

Odemba anachukua nafasi ya kocha wa zamani Godfrey ‘Solo’ Oduor ambaye alijiuzulu Agosti baada kuhudumu kwa miezi sita pekee.

Afisa wa Mawasiliano wa Shirikisho la Soka nchini (FKF) Kenn Okaka, amethibitishia Taifa Spoti habari hizo.

“Odemba ndiye kocha mkuu mpya wa Starlets. Atataja rasmi kikosi cha muda kesho Jumapili kwa sababu mchakato wa kuteua kikosi cha kudumu unaendelea. Baadhi ya wachezaji tayari wamepata mwaliko lakini tusubiri hadi kila kitu kitakapokuwa rasmi,” alisema Okaka.

Huku wachezaji wakisubiri kwa hamu kutajwa kwenye kikosi cha muda, mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) Vihiga Queens, wamethibitisha kuwa wachezaji wao wawili; Phoebe Oketch (beki) na Janet Moraa Bundi (mshambulizi) wamejumuishwa kwenye kikosi hicho.

“Tunachukua fursa hii ya mapema kuwapongeza wachezaji wetu wawili kwa kuitwa kwenye timu ya Taifa. Tunawatakia kila la kheri katika jukumu lenu. Tunaomba mupeperushe si tu klabu zetu bali bendera ya nchi nzima juu zaidi,” taarifa ya klabu ilisoma.

Starlets itamenyana na Indomitable Lionesses ya Cameroon mnamo Septemba 22, 2023 katika mkondo wa kwanza wa shindano hilo.

Baadae mnamo Septemba 26, 2023, Starlets itakuwa wenyeji wa Cameroon jijini Nairobi.

Starlets wanatarajiwa kuripoti kambini Septemba 10, 2023.

  • Tags

You can share this post!

EACC yamulika magavana 21

Sakaja asimama upande wa wachuuzi CBD

T L