• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 8:50 AM
Kocha Bielsa afutwa kazi baada ya Spurs kuponda Leeds 4-0

Kocha Bielsa afutwa kazi baada ya Spurs kuponda Leeds 4-0

Na MASHIRIKA

KOCHA Marcelo Bielsa ametimuliwa ugani Elland Road baada ya Leeds United kupokezwa kichapo kinono cha 4-0 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi.

Klabu ya Leeds imetangaza kumfuta kazi leo Jumapili.

Mkufunzi huyo raia wa Argentina mwenye umri wa miaka 66 tayari alikuwa na presha ya kupigwa kalamu kutokana na msururu wa matokeo duni ya Leeds hata kabla ya kuongoza vijana wake kushuka dimbani kuvaana na Spurs.

Matokeo dhidi ya Spurs yaliacha Leeds katika nafasi ya 16 kwa alama 23 kwenye msimamo wa jedwali la EPL na sasa wako katika hatari ya kuteremshwa ngazi iwapo watashindwa kuhimili presha kutoka kwa Everton, Watford, Burnley na Norwich City.

Wasimamizi wakuu wa Leeds tayari wameanza kusaka kocha atakayemrithi Bielsa.

Mbali na Jesse Marsch ambaye ni mkufunzi wa zamani wa RB Leipzig, kocha mwingine anayehusishwa pakubwa na mikoba ya Leeds ni Carlos Corberan wa Huddersfield.

Masaibu ya Leeds yalianza Januari 2022 baada ya wanasoka wao tegemeo Kalvin Phillips na Patrick Bamford kupata majeraha mabaya.

Ingawa walishinda West Ham United ugani London mwezi Januari, Leeds wamejizolea alama moja pekee kutokana na mechi sita huku wakifungwa mabao 20 kutokana na michuano mitano iliyopita.

Kibarua chao ligini kilifanywa kuwa kigumu zaidi baada ya kukutanishwa na Manchester United, Liverpool na Spurs kwa usanjari huo katika mechi tatu zilizopita.

Zaidi ya kufungwa mabao sita na Liverpool ugani Anfield, Leeds walipachikwa mabao manne katika mechi dhidi ya Man-United na Spurs. Kabla ya hapo, walikuwa wamefungwa mabao matatu dhidi ya Everton na Aston Villa. Ina maana kwamba mabao 20 kati ya 60 ambayo Leeds wamefungwa kufikia sasa msimu huu yametokea mwezi Februari pekee.

Leeds ndicho kikosi cha pili katika historia ya soka ya EPL kuwahi kufungwa mabao matatu au zaidi katika kila mechi tano mfululizo za kipute hicho.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Canada yazima ndege za Urusi katika anga yake

Mbappe afikia rekodi ya Ibrahimovic katika ufungaji wa...

T L