• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 PM
Mbappe afikia rekodi ya Ibrahimovic katika ufungaji wa mabao PSG

Mbappe afikia rekodi ya Ibrahimovic katika ufungaji wa mabao PSG

Na MASHIRIKA

KYLIAN Mbappe alifunga mabao mawili na kuchangia jingine katika ushindi wa 3-1 uliosajiliwa na Paris Saint-Germain (PSG) dhidi ya Saint-Etienne katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo Jumamosi.

Lionel Messi alichangia mabao yote ya Mbappe katika dakika za 42 na 47 mtawalia. Danilo Pereira alijaza kimiani goli la tatu la PSG lililochangiwa na Mbappe kunako dakika ya 52. St-Etienne walifutiwa machozi na Denis Bouanga.

Ushindi wa PSG uliwawezesha kufungua pengo la alama 16 kati yao na Nice pamoja na Olympique Marseille kileleni mwa jedwali la Ligue 1.

Mabao ya Mbappe, 23, yalimfanya kufikia rekodi ya kigogo Zlatan Ibrahimovic anayeshikilia nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote kambini mwa PSG (mabao 156). Orodha hiyo inaongozwa na nyota wa Uruguay ambaye sasa anachezea Manchester United, Edinson Cavani kwa mabao 200.

PSG walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kujinyanyua baada ya Nantes kuwazamisha kwa mabao 3-1 katika mechi ya awali ligini.

St-Etienne sasa wanakamata nafasi ya 16 kwa alama 22, moja pekee mbele ya Troyes, Lorient, Metz na Bordeaux wanaovuta mkia wa jedwali la Ligue 1. Hofu zaidi kwa St-Etienne ni kwamba wamesakata mchuano mmoja zaidi kuliko 25 ambazo zimetandazwa na vikosi hivyo vya mwisho kwenye msimamo wa jedwali.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kocha Bielsa afutwa kazi baada ya Spurs kuponda Leeds 4-0

TAHARIRI: Kongamano la mazingira lije na ufumbuzi wa...

T L