• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Kocha Firat aitaka Stars ikung’ute Uganda, Rwanda

Kocha Firat aitaka Stars ikung’ute Uganda, Rwanda

Na CECIL ODONGO

Mkufunzi wa Harambee Stars Engin Firat, amewataka vijana wake wajikakamue ili washinde mechi zao mbili za kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Uganda na Rwanda wiki hii.

Kenya imeratibiwa itatifuana na Uganda mnamo Alhamisi katika uga wa St Mary Kitende kabla ya kutamatisha mechi yao ya kundi E dhidi Rwanda nyumbani mnamo Jumapili.Vijana wa Firat wanatarajiwa kuondoka nchini leo jioni hadi Uganda kabla ya mtanange huo.

Hata hivyo, Kenya haina nafasi ya kuelekea Qatar kwa kuwa ina alama mbili pekee.Uganda kwa upande mwingine inalenga kufuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia yake huku ikihitaji mno ushindi katika mechi hiyo kuimarisha nafasi yake.

‘Nimeteua kikosi ambacho ni mchanganyiko wa wachezaji wazoefu na wale ambao ni chipukizi. Cha msingi ni kwamba tunafaa tushinde mechi zetu mbili zilizosalia ili kumaliza vizuri hata kama hatuendi popote,’ akasema Firat jana baada ya timu hiyo kuandaa mazoezi katika uga wa Nyayo.

Mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 51 alifichua kuwa atawakosa mabeki, Brian Mandela, Joseph Okumu, kiungo Boniface Muchiri na mvamizi Masud Juma ambao wanauguza jeraha. Beki wa Simba SC Joash Onyango naye atasalia na timu yake baada ya kuruhusiwa na kocha huyo.

Kauli ya kocha huyo kuwa anapanga kujenga na kuimarisha kikosi hicho kwa siku zijazo nayo imefasiriwa kuwa huenda akaendelea kuongoza Harambee Stars hata baada ya kandarasi yake ya miezi miwili kukamilika mwezi huu.

‘Lazima baada ya mechi hizi tulenge kuwatambua wachezaji wetu wenye talanta wanaoshiriki ligi ya nje na ya ndani. Kenya ina wachezaji wazuri ambao wakitambuliwa na kufanya mazoezi pamoja kwa siku nyingi basi nchi hii itafanya vizuri katika mchezo huu,’ akaongeza.

Naye nahodha wa Harambee Stars Michael Olunga aliwataka wachezaji wenzake wajitume zaidi akisema michuano dhidi ya Uganda huwa ni mtihani mkubwa sana kwa Kenya. Katika mechi ya mkondo wa kwanza hapa nchini, Uganda na Kenya Septemba 2 ziliumiza nyasi bure kwa kutoka sare tasa.

‘Ni vizuri kocha amewapa wachezaji wachanga nafasi na ni vyema iwapo kila moja wetu atajituma ili tumalize vizuri tu katika kundi letu. Uganda ni timu ngumu na inalenga kufuzu Kombe la Dunia ila ni vyema kuwa sisi pia tujikaze na kuwashinda kwao,’ akasema mwanadimba huyo wa zamani wa Gor Mahia.

Timu itakayomaliza katika kilele cha Kundi E itajiunga na viongozi wa makundi tisa kufuzu kwa raundi ya mwisho ambapo washindi watano wataelekea Qatar kushiriki kombe la dunia mnamo Juni mwaka ujao.

You can share this post!

Bandari yalaumu uhuni wa wafuasi Homeboyz

Nebulas wafinya Little Prince vikapu vya Ligi ya Kitaifa...

T L