• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
Bandari yalaumu uhuni wa wafuasi Homeboyz

Bandari yalaumu uhuni wa wafuasi Homeboyz

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

MENEJA wa timu ya Bandari FC, Albert Ogari amelaumu vitendo alivyodai vya kihuni vilivyotekelezwa na mashabiki wa Kakamega Homeboys FC mwishoni mwa mechi yao ya Ligi Kuu ya FKF iliyofanyika katika uwanja wa Bukhungu juzi Jumapili.

Ogari alisema vitendo hivyo vya mashabiki kuvamia uwanja na kutaka kuwajeruhi wachezaji na mashabiki wa Bandari FC baada ya kukamilika kwa mchezo huo uliokuwa na matokeo ya kufungana bao 1-1, havikuwa vizuri na havifai kufanyika katika karne hii.

“Mchezo wa soka wakati huu unastahili kuchezwa kistaarabu na timu kukubali matokeo yoyote yale yanayotokea kiwanjani lakini kwa mashabiki kuingia kiwanjani na kufanya vitendo vya kihuni, ni jambo ambalo halifai kufanyika,” akasema meneja huyo.

Ogari alisema hakuna wakati mmoja mashabiki wao wamewahi kutekeleza vitendo kama vilivyotekelezwa na wafuasi wa Homeboys hata kama matokeo ya mechi yao ya nyumbani yanakuwa mabaya.

“Nimeshangaa mno kwamba ilikuwa ni sisi ndio tulalamike kwa jinsi mechi hiyo ilivyochezeshwa kwani wapinzani wetu wamekuwa na siku njema ya kusaidiwa kwa kila njia na mpaka kupewa penalti iliyokuwa haistahili dakika za majeruhi ambayo waliipoteza,” akasema.

Kocha wa Bandari FC, Andre Cassa Mbungo anasema anamshukuru Mungu kwamba wachezaji pamoja na maafisa wa timu hiyo waliondoka na kurudi nyumbani salama “Hakika tulijitahidi kuvuka sehemu ambayo ingelituletea matatizo mengi na kuwa na majeruhi wengi,” akasema Mbungo.

You can share this post!

Westham tayari kung’ang’ania ligi kuu uingereza

Kocha Firat aitaka Stars ikung’ute Uganda, Rwanda

T L