• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Kocha Gregg Berhalter aliyetimuliwa kwa kumpiga mkewe mateke hatimaye arejeshwa kazini

Kocha Gregg Berhalter aliyetimuliwa kwa kumpiga mkewe mateke hatimaye arejeshwa kazini

Na MASHIRIKA

GREGG Berhalter ameteuliwa upya kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Amerika, miezi sita baada ya mkataba wake kutamatika huku akifanyiwa uchunguzi kuhusu mienendo yake ya awali.

Mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 49 alikuwa amedhibiti mikoba ya Amerika kwa kipindi cha miaka minne alipokiri kumpiga mateke mkewe akiwa tineja.

Berhalter alichunguzwa na US Soccer, shirika ambalo hatimaye lilibaini kuwa “halikuwa na uwezo wowote wa kisheria kuzuia kuajiriwa kwake.”

Ilivyo, Berhalter sasa ataongoza Amerika kwa fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazoandaliwa kwa pamoja na Amerika, Mexico na Canada.

Aliongoza Amerika kutinga hatua ya 16-bora kwenye fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar ambapo walitandikwa na Uholanzi 3-1.

Madai dhidi yake kwamba alimdhulumu mkewe yalitolewa mwezi wa Disemba 2022 huku mkataba wake wa awali ukitarajiwa kukatika rasmi mwishoni mwa mwezi huo.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, baada ya kutia saini mkataba huku akiwa na mkewe Rosalind, Berhalter alielezea tukio hilo la 1992 ambapo aliripotiwa kumdhulumu mkewe huku akishikilia kwamba “hapakuwa na kijisababu chochote cha yeye kufanya hivyo”.

BJ Callaghan baadaye alipokezwa mikoba ya Amerika na anatarajiwa kusimamia fainali ya Concacaf Nations League jijini Las Vegas na fainali ya kivumbi cha Concacaf Gold Cup kitakachoanza baadaye mwezi huu.

Rosalind ni mama wa kiungo mzoefu wa Borussia Dortmund na Amerika, Giovanni Reyna. Mrembo huyo amesema alimshtaki Berhalter kuhusu kisa hicho cha 1992 mnamo Disemba 11, 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Giroud na Mbappe wabeba Ufaransa dhidi ya Gibraltar kwenye...

Wabunge waliokwepa kushiriki kura muhimu

T L