• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 3:13 PM
Kocha Joachim Loew hatimaye kuagana na timu ya taifa ya Ujerumani baada ya kuinoa kwa miaka 15

Kocha Joachim Loew hatimaye kuagana na timu ya taifa ya Ujerumani baada ya kuinoa kwa miaka 15

Na MASHIRIKA

KOCHA wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Loew, 61, atajiuzulu mwishoni mwa kampeni za kuwania taji la Euro 2021.

Mkufunzi huyo alitwaa mikoba ya Ujerumani mnamo 2006 na amesimamia jumla ya michuano 189 kufikia sasa kambini mwa miamba hao wa soka waliotwazwa mabingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2014 nchini Brazil.

Anajivunia pia kuongoza Ujerumani kunyayua ufalme wa Confederations Cup mnamo 2017 na kutinga fainali ya Euro 2008 ambapo walizidiwa maarifa na Uhispania. Chini ya Loew, Ujerumani walibanduliwa mapema kwenye fainali za Kombe la Dunia za 2018 nchini Urusi katika hatua ya makundi.

“Nachukua hatua hii (ya kujiuzulu) nikiwa mwingi wa fahari. Napongeza vinara wa Shirikisho la Soka la Ujerumani kwa kuniaminia mikoba ya kikosi hicho ambacho kwa sasa nalenga kukiongoza kunyakua taji la Euro 2021,” akatanguliza Loew.

“Ninajivunia mambo mengi ambayo kikosi kimefanikiwa kufanya chini yangu kwa muda wote ambao nimekuwa kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani. Mengi tuliyofanya pamoja yanazidi ufanisi wa kutwaa Kombe la Dunia mnamo 2014,” akasema kwa kuongeza kwamba tija zaidi kwake ni kuweza kufanya kazi na wanasoka bora zaidi nchini Ujerumani kwa takriban miaka 17.

Loew ambaye ni kiungo wa zamani wa kikosi cha SC Freiburg katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), alikuwa kocha msaidizi wa Ujerumani chini ya mkufunzi Jurgen Klinsmann kati ya 2004 na 2006.

Tangu apokezwe mikoba, Loew ameongoza Ujerumani kushinda jumla ya mechi 120 na kufunga wapinzani mabao 448.

Kichapo cha 6-0 ambacho Ujerumani walipokezwa na Uhispania katika gozi la UEFA Nations League mnamo 2020, kiliwafanya mashabiki kumshinikiza Loew kujiuzulu huku maamuzi yake ya kuwatema wanasoka Mats Hummels, Jerome Boateng na Thomas Muller kikosini yakichochea hasira ya mashabiki kutaka Shirikisho la Soka la Ujerumani kumpiga kalamu.

Ujerumani kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Iceland, Romania na North Macedonia kwa usanjari huo katika juhudi za kufuzu kwa Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Kikosi hicho tayari kimetiwa katika ‘Kundi la Kifo’ linalojumuisha Hungary, mabingwa watetezi wa Euro Ureno na mabingwa wa Kombe la Dunia Ufaransa kwenye fainali za Euro mwaka huu wa 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wakulima wa pamba Machakos wapata nguvu kujiimarisha zaidi

Visa vya wizi wa mifugo vyazidi katika kijiji cha Maguguni...