• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Wakulima wa pamba Machakos wapata nguvu kujiimarisha zaidi

Wakulima wa pamba Machakos wapata nguvu kujiimarisha zaidi

Na LAWRENCE ONGARO

WAKULIMA wa eneo la Ndalani, Yatta kaunti ya Machakos, wametabasamu baada ya kupokea pamba aina ya BT iliyozinduliwa huko.

BT inatajwa kama yenye kustahimili mazingira ya maeneo kame.

Mkurungenzi wa kiwanda cha Thika Cloth Mills Limited Bi Tejal Dodhia ametaja zao hilo kama spesheli kwa sababu hiyo ya kustahimili maeneo yenye ukame.

Alisema mbegu yake pia ni ya bei nafuu inayotoa mazao ya hali ya juu.

“Tulikuwa tunalazimika kusafiri hadi nchi jirani kama Tanzania kununua pamba lakini wakati huu tutajitegemea hapa nchini,” alisema Bi Dodhia.

Alishukuru serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kwa kuendeleza Ajenda Nne muhimu za serikali.

Alieleza kuwa tayari alipata zabuni kupitia serikali kushona nguo za Jeshi jambo alilotaja kama mwelekeo unaofaa.

“Ilibidi niendelee kuajiri wafanyakazi baada ya kuwa nyumbani kwa miezi kadha wakati wa mlipuko wa corona,” alisema mkurugenzi huyo.

Alitoa wito kwa serikali kupitia Waziri wa Kilimo kuhakikisha wakulima wanapata mbegu za kutosha ili kupanda pamba kwa wingi.

Aliyasema hayo alipozuru eneo la Ndalani, Yatta, kuwahamasisha wakulima jinsi ya kupanda mbegu hiyo ya pamba.

Wakati huo pia wakulima hao waliwachagua maafisa wapya watakaoendesha shughuli za kilimo cha pamba katika Kaunti ya Machakos.

Mkulima wa pamba katika Kaunti ya Machakos. Picha/ Lawrence Ongaro

Naibu Gavana wa Machakos Bw Francis Maliti alisema kaunti hiyo itatoa tingatinga 40 kulimia wakulima hao wa pamba.

“Tuna furaha kuletewa wataalam wa zao hilo ambao wamewahamasisha wakulima wetu jinsi ya kupanda pamba kwa kutumia mbinu na ujuzi wa kisasa,” alisema Bw Maliti.

Alitoa wito kwa serikali kuwaleta maafisa wa kilimo ambao watazuru maeneo hayo ili kufahamu jinsi kilimo kinavyoendeshwa.

Mwakilishi wa wakulima hao katika eneo la Yatta, Bw Francis Kilango aliwahimiza wakazi wa eneo hilo kuzingatia upanzi wa pamba kwa sababu itamaliza umaskini katika eneo lote la Kaunti ya Machakos na maeneo jirani.

“Tayari tumepata maafisa wapya wenye maono ambao watawapa mwongozo wakulima hao jinsi ambavyo wanaweza kujiendeleza kwa kupanda pamba,” alisema Bw Kilango.

Alisema kwa miaka mingi wakazi wa Yatta wamekuwa wakitegemea chakula cha msaada, lakini baada ya kugeuza mkondo wa kupanda pamba bila shaka mambo yatageuka.

Alisema kiwanda cha Thika Cloth Mills kitajitolea kununua pamba yote ya eneo hilo huku wakulima wakifaidika kifedha.

Alizidi kueleza ya kwamba mwaka 2020, aliandamana na mkurugenzi wa Thika Cloth Mills Bi Dodhia, na kuzuru hadi maeneo ya Homa Bay, Kisumu, na Siaya ili kuwahamasisha wakulima kupanda pamba kwa wingi.

You can share this post!

Madhara yaletwayo na uvaaji wa viatu vyenye visigino virefu...

Kocha Joachim Loew hatimaye kuagana na timu ya taifa ya...