• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
Kocha Ten Hag ateua wakufunzi watakaomsaidia kunoa kikosi cha Man-United

Kocha Ten Hag ateua wakufunzi watakaomsaidia kunoa kikosi cha Man-United

Na MASHIRIKA

ERIK Ten Hag atasaidiana na Steve McClaren na Mitchell van der Gaag kudhibiti mikoba ya Manchester United.

Wawili hao wamewahi kufanya kazi pamoja na Ten Hag nchini Uholanzi – McClaren kambini mwa FC Twente na Van der Gaag kambini mwa Ajax.

McClaren ambaye ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza aliwahi kuwa msaidizi wa kocha Alex Ferguson kambini mwa Man-United kwa zaidi ya misimu miwili kati ya 1999 na 2001. Van der Gaag kwa upande wake alikuwa msaidizi wa Ten Hag kwa mwaka mmoja uliopita katika kikosi cha Ajax.

Ten Hag amesema kuwa hajajidunisha kitaaluma kwa kukubali kunoa Man-United.

Mkufunzi huyo raia wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 52 ndiye kocha wa tano kupokezwa mikoba ya Man-United kwa kandarasi ya kudumu tangu Sir Alex Ferguson astaafu mnamo 2013.

“Sioni kama nahatarisha sifa zote nzuri nilizo nazo katika ulingo wa ukufunzi. Man-United ni klabu yenye historia ndefu. Sasa ni wakati wa kutazama mbele na kusuka mambo kwa ajili ya siku za usoni,” akasema.

Ten Hag pia alidokeza kwamba fowadi Cristiano Ronaldo hatabanduka ugani Old Trafford huku akisisitiza kwamba anatarajia mabao kutoka kwa Ureno huyo muhula ujao.

Ten Hag ambaye ni kocha wa zamani wa Ajax, alikuwa akizungumza na wanahabari wakati wa kutambulishwa kwake rasmi kwa mashabiki, usimamizi na wachezaji wa Man-United saa chache baada ya kuhudhuria mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ulioshuhudia waajiri wake wapya wakipokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Crystal Palace ugani Selhurst Park.

Man-United walikamilisha kampeni za EPL msimu huu katika nafasi ya sita jedwalini kwa alama 58 ambayo ni idadi ndogo zaidi tangu 1989-90. Hata hivyo, walifuzu kwa Europa League msimu wa 2022-23.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

FAO yafanya majaribio ya mpango wa kudhibiti shughuli za...

Ulinzi Starlets pazuri kumaliza katika nafasi ya pili KWPL

T L