• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uholanzi wasubiri hadi dakika za mwisho kuzamisha chombo cha Senegal

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uholanzi wasubiri hadi dakika za mwisho kuzamisha chombo cha Senegal

Na MASHIRIKA

MABAO mawili ya haraka mwishoni mwa kipindi cha pili kutoka kwa Cody Gakpo na Davy Klaassen yaliwezesha Uholanzi kuvuna ushindi muhimu wa 2-0 dhidi ya Senegal katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi A mnamo Jumatatu.

Gakpo ambaye ni fowadi wa PSV Eindhoven alimwacha hoi kipa Edouard Mendy katika dakika ya 84 kabla ya Klaassen kushirikiana vilivyo na Frenkie de Jong zikisalia sekunde chache kwa mchezo kukamilika.

Mshambuliaji wa Uholanzi #08 Cody Gakpo asherehekea baada ya kufunga bao la kwanza la Uholanzi wakicheza dhidi ya Senegal katika Kundi A kwenye mashindano ya Kombe la Dunia uwanjani Al-Thumama jijini Doha nchini Qatar mnamo Novemba 21, 2022. PICHA | AFP

Kocha Louis van Gaal aliwaleta ugani wachezaji Klaassen na Memphis Depay katika kipindi cha pili na wakachangia pakubwa kubadilisha kasi ya mchezo iliyodhibitiwa na Senegal kwa kipindi kirefu ugani Al Thumama.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Senegal kufungwa bao kutokana na mechi saba. Wafalme hao wa Afrika walianza mchezo kwa matao ya juu ila wakapoteza nafasi nyingi za wazi kupitia kwa Boulaye Dia, Idrissa Gueye na Papa Gueye waliomtatiza pakubwa kipa wa Uholanzi, Andries Noppert.

Kwa kushinda Senegal, Uholanzi kwa sasa wanalenga kukomoa Ecuador na wenyeji Qatar katika michuano mingine miwili ya Kundi A na kujipa uhakika wa kukamilisha kampeni za kundi hilo wakiwa kileleni. Ecuador walifungua Kundi A kwa ushindi muhimu wa 2-0 dhidi ya Qatar ugani Al Bayt mnamo Novemba 20, 2022.

Senegal waliokosa huduma za fowadi Sadio Mane anayeuguza jeraha la mguu, walishuka dimbani wakiwa na presha ya kuzamisha Uholanzi ili kuweka hai matumaini ya mojawapo ya timu za Afrika kusonga zaidi ya hatua ya robo-fainali kwenye historia ya fainali za Kombe la Dunia.

Ni mataifa matatu pekee kutoka Afrika ambayo yamewahi kutinga hatua ya nane-bora kwenye Kombe la Dunia – Cameroon (1990), Senegal (2002) na Ghana (2010).

Mane ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Liverpool, alipata jeraha akichezea waajiri wake wa sasa, Bayern Munich, katika mechi ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) dhidi ya Werder Bremen mwanzoni mwa Novemba 2022.

Nyota huyo alifunga penalti dhidi ya Misri na kuzolea Senegal Kombe la Afrika (AFCON) mnamo Februari 2022, mwezi mmoja kabla ya kuongoza taifa lake kuzamisha Misri kwa mara nyingine na kujikatia tiketi ya kunogesha Kombe la Dunia kwa mara ya tatu.

Kutokuwepo kwake kuliacha kocha Aliou Cisse katika ulazima wa kutegemea zaidi maarifa ya Ismaila Sarr na Famara Diedhiou walioshirikiana na Iliman Ndiaye, Bamba Dieng na Krepin Diatta katika safu ya mbele ya Senegal.

Senegal sasa wana kibarua cha kulaza Qatar na kuzamisha Ecuador katika michuano inayofuata kadri wanavyolenga kutinga raundi ya muondoano kwa mara nyingine baada ya Uturuki kuwadengua kwa 1-0 kwenye robo-fainali za 2002 nchini Japan.

Uholanzi wanajivunia ufufuo mkubwa wa makali yao chini ya kocha Van Gaal aliyewaongoza kufuzu kwa fainali za UEFA Nations League mwaka huu, hiyo ikiwa mara yao ya pili baada ya makala matatu.

Wanafainali hao wa Kombe la Dunia 2010, walikosa kipute cha Urusi mnamo 2018 baada ya kutinga nusu-fainali za 2014 nchini Brazil wakinolewa na Van Gaal.

Uholanzi ni miongoni mwa timu kubwa katika ulingo wa soka ambazo hazijawahi kunyanyua Kombe la Dunia. Kikosi hicho kilipoteza fainali ya 1974, 1978 na 2010 dhidi ya Ujerumani (2-1), Argentina (3-1) na Uhispania (1-0) mtawalia. Argentina iliwabandua kwa penalti 4-2 kwenye nusu-fainali za 2014 baada ya sare tasa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

GMO: Wanasayansi watoa kauli kinzani

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Gareth Bale aongoza Wales...

T L