• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Gareth Bale aongoza Wales kulazimishia Amerika sare ya 1-1 katika Kundi B

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Gareth Bale aongoza Wales kulazimishia Amerika sare ya 1-1 katika Kundi B

Na MASHIRIKA

GARETH Bale alifunga penalti kunako dakika ya 82 na kusaidia timu ya taifa ya Wales kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Amerika katika pambano la Kundi B kwenye Kombe la Dunia mnamo Jumatatu uwanjani Ahmad Bin Ali, Al Rayyan.

Wales wanashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 1958 huku Amerika wakirejea ulingoni kutandaza soka ya kipute hicho baada ya kukosa kunogesha fainali za 2018 zilizotamalakiwa na Ufaransa nchini Urusi.

Japo USA wametinga raundi ya muondoano kwenye Kombe la Dunia mara nne kutokana na fainali saba zilizopita, hawajawahi kushinda kikosi kutoka bara Ulaya katika majaribio tisa ya awali.

Wales kwa upande wao sasa hawana ushindi wowote tangu walaze Ukraine 1-0 mnamo Juni 2022 kwenye mchujo wa kuwania tiketi ya kuelekea Qatar kunogesha makala ya 22 ya Kombe la Dunia.

Kocha Robert Page alimleta ugani fowadi Kieffer Moore aliyechochea kasi ya mchezo kwa upande wa Wales huku ushirikiano mkubwa kati yake na Ben Davies ukiwa mwiba kwa mabeki wa Amerika.

 

Mshambuliaji wa Wales Gareth Bale aabiri basi mara baada ya kushuka kutoka kwa ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamad jijini Doha mnamo Novemba 16, 2022. PICHA | AFP

Penalti ambayo Wales walipewa katika kipindi cha pili ilitokana na tukio la Bale kuchezewa na Walker Zimmerman visivyo ndani ya kijisanduku.

Wales watarejea ugani Ahmad Bin Ali mnamo Novemba 25, 2022 kuvaana na Iran wanaohitaji muujiza kujinyanyua baada ya Uingereza kuwapepeta 6-2 mnamo Jumatatu jioni uwanjani Khalifa International. Masogora wa Page watafunga kampeni zao za Kundi B dhidi ya Uingereza mnamo Novemba 29, 2022.

Wales walikomesha subira ya miaka 58 kufuzu kwa fainali za soka ya haiba kubwa mnamo 2016 kwa kujikatia tiketi ya kunogesha mashindano ya Euro ambayo waliyaaga katika hatua ya nusu-fainali. Walidhihirisha tena ubabe wao miaka minne baadaye kwa kutinga raundi ya muondoano kwenye fainali za Euro 2020.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uholanzi wasubiri hadi dakika za...

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Mabingwa watetezi Ufaransa...

T L