• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 11:02 AM
Kun Aguero ni mali rasmi ya Barcelona

Kun Aguero ni mali rasmi ya Barcelona

Na MASHIRIKA

SASA ni rasmi kwamba fowadi Sergio Kun Aguero anajiunga na Barcelona kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kandarasi yake ya sasa na Manchester City kutamatika mwishoni mwa Juni 2021.

Sogora huyo mwenye umri wa miaka 32 anaondoka Man-City baada ya kuhudumu kambini mwa miamba hao wa soka ya Uingereza kwa kipindi cha miaka 10 ambapo aliweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote kwa kupachika wavuni mabao 260 kutokana na mechi 390.

Mechi ya mwisho kwa Aguero kuchezea Man-City ni ile iliyomshuhudia akitokea benchi dhidi ya Chelsea kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Mei 29, 2021 jijini Porto, Ureno.

“Hakuna asiyejua kwamba Barcelona ndiyo klabu bora zaidi duniani. Naamini kwamba nilifanya maamuzi mazuri ya kujiunga na kikosi hicho na hiyo ni hatua kubwa zaidi katika maendeleo yangu kitaaluma,” akasema Aguero.

“Nina matarajio ya kuzoea haraka maisha uwanjani Camp Nou na kusaidia Barcelona kuanza kushinda mataji ya haiba,” akaongeza mchezaji huyo wa zamani wa Atletico Madrid.

Kikosi chochote kitakachokuwa na azma ya kumsajili Aguero kutoka Barcelona kitalazimika kuweka mezani kima cha Sh12 bilioni kabla ya mkataba wake wa miaka miwili kukamilika kambini mwa klabu hiyo.

Akiwa Man-City, Aguero ambaye kwa sasa ataungana na Lionel Messi ambaye ni mvamizi mwenzake katika timu ya taifa ya Argentina, alijizolea jumla ya mataji 15.

Barcelona walikamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo 2020-21 katika nafasi ya tatu nyuma ya Real Madrid na mabingwa Atletico wanaojivunia huduma za aliyekuwa nyota wao, Luis Suarez. Suarez ambaye ni raia wa Uruguay, aliondoka Barcelona na kutua Atletico kwa kima cha Sh728 milioni mwishoni mwa msimu wa 2019-20.

Chini ya kocha Ronald Koeman, Barcelona walibanduliwa na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa kwenye hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu. Hata hivyo, walijizolea taji la Copa del Rey baada ya kupepeta Athletic Bilbao 4-0 kwenye fainali iliyowakutanisha mnamo Aprili, 2021.

Messi aliibuka mfungaji bora wa Barcelona mnamo 2020-21 kwa mabao 38 huku wanasoka wawili raia wa Ufaransa – Antoine Griezmann na Ousmane Dembele wakipachika wavuni mabao 20 na 11 mtawalia.

Aguero anaondoka EPL akishikilia nafasi ya nne kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote kwa magoli 184. Japo Chelsea walikuwa pia wakimezea huduma za Aguero, nyota huyo alihiari kurejea Uhispania kusakata soka ya La Liga – kipute kilichowahi kumpa fursa ya kupachika wavuni mabao 74 akivalia jezi za Atletico kwa misimu mitano kabla ya kuyoyomea Man-City kwa kima cha Sh5 bilioni mnamo 2011.

Beki Eric Garcia wa Man-City na kiungo Georginio Wijnaldum wa Liverpool ni wachezaji wengine wawili wanaohusishwa pakubwa na Barcelona muhula huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wamalwa ahusishwa na chama kipya cha DAP-K kilichosajiliwa

Fowadi wa zamani wa Brighton na Palace, Glenn Murray,...