• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Lazio watia kapuni alama tatu za bwerere Serie A baada ya Torino kuingia mitini

Lazio watia kapuni alama tatu za bwerere Serie A baada ya Torino kuingia mitini

Na MASHIRIKA

MECHI ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) iliyokuwa iwakutanishe Lazio na Torino iliwapa wenyeji alama tatu za bwerere baada ya wageni Torino kukosa kusafiri uwanjani Olimpico, Roma baada ya maafisa wa afya kutia kikosi kwenye karantini.

Baada ya wanasoka wanane wa Torino kupatikana na virusi vya corona, maafisa wa afya jijini Turin, Italia waliomba kikosi hicho cha Torino kutosafiri mjini Roma kuvaana na Lazio.

Hata hivyo, vinara wa Serie A walitaka mchuano huo usakatwe jinsi ilivyoratibiwa licha ya gozi la awali lililokuwa liwakutanishe Torino na Sassuolo kusitishwa siku tano kabla ya tarehe ambapo vikosi hivyo vilitarajiwa kushuka dimbani.

Licha ya hali iliyowasibu Torino waliokuwa zaidi ya kilomita 680 kutoka mjini Roma, Lazio walikitaja kikosi chao kwa ajili ya mechi hiyo iliyokuwa isakatwe mnamo Machi 2, 2021.

Kutibuka kwa mechi hiyo kulirejesha kumbukumbu za Oktoba 2020 ambapo mechi iliyokuwa iwakutanishe Juventus na Napoli ilikosa kufanyika kwa sababu ya corona japo Juventus wakapokezwa alama zote tatu.

Kwa mujibu wa kanuni za Serie A, Lazio wanatarajiwa kupokezwa alama tatu za bure na ushindi wa 3-0 huku Torino wakiondolewa alama moja kwa kukataa kufika uwanjani kwa ajili ya mechi kati yao na Lazio.

Hata hivyo, Napoli walikata rufaa kwenye Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki ya Italia (CONI) baada ya kuondolewa alama na sasa wakapangiwa upya kucheza na Juventus ambao ni mabingwa watetezi wa Serie A.

Torino kwa sasa hawajawahi kucheza mechi yoyote tangu wapige Cagliari 1-0 mnamo Februari 19, 2021. Mchuano wao ujao ni dhidi ya Crotone wanaovuta mkia. Mechi hiyo itasakatwa mnamo Machi 7, 2021.

Lazio watakutakana na Juventus jijini Turin mnamo Machi 6. Watashuka dimbani kwa ajili ya mechi hiyo wakilenga kujinyanyua baada ya kupokezwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Bologna mnamo Februari 27, siku chache baada ya kucharazwa 4-1 na Bayern Munich kwenye mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko atimuliwa kwa ubakaji...

Iheanacho anusuru Leicester dhidi ya Burnley