• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 3:41 PM
Iheanacho anusuru Leicester dhidi ya Burnley

Iheanacho anusuru Leicester dhidi ya Burnley

Na MASHIRIKA

FOWADI Kelechi Iheanacho aligeuka tegemeo la Leicester City dhidi ya Burnley katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyomshuhudia kocha Brendan Rodgers akikosa huduma za wanasoka wengi wa haiba kubwa katika kikosi chake cha kwanza.

Kutokuwepo kwa Harvey Barnes na James Maddison wanaouguza majeraha kulimsaza Iheanacho katika ulazima wa kuongoza safu ya mbele ya Leicester kwa ushirikiano na Jamie Vardy aliyekuwa akiwajibishwa katika mechi ya pili mfululizo tangu apone jeraha.

Masihara ya beki Hamza Choudhury yalimpa fowadi Matej Vydra fursa ya kuwafungia Burnley bao katika dakika ya nne kabla ya Iheanacho kusawazisha kunako dakika ya 34 na kufanya pambano hilo kukamilika kwa sare ya 1-1.

Kila kikosi kilikuwa na nafasi nyingi za wazi kufunga mabao zaidi katika mechi hiyo iliyoshuhudia makipa Nick Pope wa Burnley na Kasper Schmeichel wa Leicester wakijituma vilivyo.

Scheichel alipangua makombora mazito aliyoelekezewa na James Tarkowski na Chris Wood huku Pope akizidhibiti vilivyo fataki kutoka kwa Youri Tielemens na Vardy.

Japo alama iliyovunwa na Burnley kutokana na mechi hiyo iliwadumisha katika nafasi ya 15, iliwawezesha kufungua pengo la alama kati yao na nambari 18 Fulham kwa pointi sita zaidi. Burnley ka sasa wamejizolea alama 29 kutokana na mechi 26 zilizopita.

Kwa upande wa Leicester, sare dhidi ya Burnley iliwasaza katika nafasi ya tatu kwa alama 50, sita zaidi kuliko nambari tano Chelsea ya kocha Thomas Tuchel.

Iheanacho aliyejulikana kwa wepesi wa kutikisa nyavu za wapinzani akivalia jezi za Manchester City, alijiunga na Leicester mnamo 2017 baada ya kusajiliwa kwa kima cha Sh3.5 bilioni.

Maddison na Barnes wamefunga na kuchangia jumla ya mabao 15 ambayo yamepachikwa wavuni na Leicester kutokana na mechi 20 zilizopita za EPL.

Ushindi kwa Burnley kungewaepushia presha zaidi kutoka kwa vikosi vitano vya mwisho hasa ikizingatiwa kwamba walijibwaga ugani kwa minajili ya mechi hiyo siku tatu baada ya kupokezwa kichapo cha 4-0 kutoka kwa Tottenham Hotspur ya kocha Jose Mourinho.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Lazio watia kapuni alama tatu za bwerere Serie A baada ya...

Sheffield yapiga Aston Villa katika EPL licha ya kusalia na...