• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:55 AM
Leopards yatandika Dandora Love 6-1 mechi ya kirafiki

Leopards yatandika Dandora Love 6-1 mechi ya kirafiki

Na JOHN ASHIHUNDU

Mabingwa mara 13 wa Ligi Kuu Nchini, AFC Leopards wameandikisha ushindi mkubwa baada ya kuicharaza Dandora Love 6-1 kwenye mechi ya kirafiki iliyochezewa Camp Toyoyo, jana Alhamisi.

Leopards ilitumia mechi hiyo dhidi ya vijana hao wa Supa Ligi kujipima wakati huu timu ziko likizoni kwa wiki mbili kwa ajili ya mechi za kimataifa zinazoendelea kote duniani. Kenya haishiriki katika hizo za kimataifa kutokana na marufuku ya FIFA.

Maxwell Otieno na Brian Wanyama walifunga mawili kila mmoja, huku mabao mengine yakipatikana kupitia kwa John Makwata na Victor Omune.

Makwata ambaye Jumapili iliyopita aliifungia Leopards bao la kusawazisha dhidi ya Kenya Police kwenye ligi kuu alionyesha kiwango cha juu katika mechi hiyo ya kupimana nguvu.

Ligini, Leopards wanashikilia nafasi ya 11 baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 28 kutokana na mechi 22. Wakati huo huo, aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Tusker, AFC Leopards, Gor Mahia Joseph Wanyonyi ataongoza kikosi cha Fortune Sacco dhidi ya timu geni ya Naivas Jumamosi katika pambano la Supa Ligi linalotarajiwa kuvutia mashabiki wengi

Hata hivyo, kikosi hicho cha kocha Nicodemus Omasete kitahitaji kuzidisha bidii baada ya awali kutoka sare na Shabana katika mechi ambayo walipoteza nafasi nyingi za kufunga mabao mjini Awendo.

“Tumejiandaa vilivyo kukabiliana na Naivas. Tutaingia uwanjani kupigania ushindi kwa vyovyote vile. Wapinzani wetu ni wagumu pia lakini tuko tayari kwa pambano hilo,” alisema Omasete huku akitoa mwito kwa mashabiki wajitokeze kwa wingi kushangilia vijana wa nyumbani.

Mechi za Jumamosi ni: Coastal Heroes v Mwatata United (Mbaraki Sports Club, saa saba), Fortune Sacco v Naivas (Kianyaga Stadium), Kibera Black Stars v Mara Sugar (Camp Toyoyo), Migori Youth v Dandora Love (Migori Stadium), SS Assad v MCF (Shamu, Msambweni).

Jumapili: Gusii United v Silibwet (Green Stadium Awendo), Kisumu All Stars v Muhoroni Youth (Moi Stadium), Vihiga United v Zoo Kericho (Mumias Sports Complex).

Jumatatu: Mombasa Elite v APS Bomet (Mbaraki Sports Club).

You can share this post!

Orao: Tuna uwezo kujiondoa mduara hatari

Kenya kati ya mataifa tisa kuwania tiketi ya kushiriki...

T L