• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 11:28 AM
Lewandowski aweka rekodi mpya ya ufungaji wa mabao Bundesliga

Lewandowski aweka rekodi mpya ya ufungaji wa mabao Bundesliga

Na MASHIRIKA

ROBERT Lewandowski alifunga mara mbili na kufikisha jumla ya mabao 31 katika kampeni za Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) msimu huu.

Mvamizi huyo raia wa Poland alisaidia waajiri wake kupepeta Union Berlin 4-0 ugani Allianz Arena na hivyo kufungua mwanya wa alama saba kati yao na nambari mbili Borussia Dortmund kileleni mwa jedwali la Bundesliga.

Lewandowski kwa sasa amefunga mabao 30 na zaidi katika kampeni za Bundesliga kwa kipindi cha misimu mitano mfululizo na hivyo kufikia rekodi iliyowekwa na nguli wa Ujerumani, Gerd Muller.

Penalti yake dhidi ya Union Berlin ilifanya mambo kuwa 3-0 mwishoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya kufunga bao la nne la waajiri wake mwanzoni mwa kipindi cha pili. Magoli mengine ya Bayern yalifumwa wavuni kupitia Kingsley Coman na Tanguy Nianzou.

Coman ambaye ni raia wa Ufaransa ndiye alifungulia Bayern ukurasa wa mabao katika dakika ya 16 baada ya kumwacha hoi kipa wa Union Berlin, Andreas Luthe.

Nusura Robin Knoche na Taiwo Awoniyi wafungie Union Berlin mabao katika kipindi cha kwanza kabla ya Nianzou kutikisa nyavu za wageni wao baada ya kushirikiana na Joshua Kimmich.

Chini ya kocha Julian Nagelsmann, Bayern walishuka dimbani wakiwa na ulazima wa kushinda baada ya kupoteza mechi mbili za awali.

You can share this post!

AC Milan warejea kileleni mwa jedwali la Serie A

Impala yaendea Mwamba fainali ya Ligi Kuu ya raga ya...

T L