• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Liverpool waweka rekodi katika soka ya Ligi Kuu ya Uingereza huku wanasoka wao watatu wakiongoza orodha ya wafungaji bora EPL

Liverpool waweka rekodi katika soka ya Ligi Kuu ya Uingereza huku wanasoka wao watatu wakiongoza orodha ya wafungaji bora EPL

Na MASHIRIKA

KOCHA Jurgen Klopp amekiri kwamba itakuwa vigumu kwa washindani wao muhula huu kuzima ari ya Liverpool ambao wameweka wazi azma ya kujizolea ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Liverpool ndicho kikosi cha pekee ambacho kimetikisa nyavu za wapinzani katika kila mojawapo ya mechi 13 za EPL msimu huu. Miamba hao pia wamefunga angalau mabao mawili katika kila mojawapo ya michuano 17 iliyopita kwenye mashindano yote. Hiyo ndiyo rekodi nzuri zaidi kuwahi kusajiliwa na klabu ya EPL katika kipindi cha miaka 100.

“Kikosi kinaridhisha na kinazidi kuwa imara. Kila sogora anafahamu cha kufanya na ushindani ni wa kiwango cha juu kambini. Vijana wana azma ya kutwaa ubingwa wa mataji kadhaa na sidhani kuna kitu kitakachowapotezea dira,” akasema Klopp huku akiwa mwingi wa sifa kwa mvamizi Diogo Jota.

Kufikia sasa, Liverpool wanajivunia mabao 39 kutokana na mechi 13 zilizopita za EPL. Hiyo ndiyo idadi kubwa zaidi ya mabao kuwahi kufungwa na timu hiyo kufikia hatua kama hii kwenye kipute cha EPL. Rekodi hiyo inapita ile iliyojivuniwa na Liverpool mnamo 2019-20 walipotawazwa wafalme wa soka ya Uingereza kwa mara ya 19.

Chini ya Klopp, Liverpool walikomoa Southampton 4-0 katika gozi la EPL mnamo Jumamosi uwanjani Anfield na kuweka hai matumaini ya kutawazwa wafalme wa kipute hicho muhula huu. Sasa wametia kapuni alama 28, tano zaidi kuliko nambari tano Arsenal waliokung’uta Newcastle United 2-0 ugani Emirates.

Kinachomwaminisha zaidi Klopp ni ubabe na uwezo wa mafowadi Mohamed Salah, Sadio Mane na Jota ambaye sasa amemweka Roberto Firmino katika ulazima wa kusugua benchi. Salah ndiye anaongoza orodha ya wafungaji bora wa EPL kwa mabao 11, manne zaidi kuliko Mane na Jota wanaokamata nafasi ya pili.

Kati ya mechi 10 zilizopita ambazo zimeshuhudia Jota akipangwa katika kikosi cha kwanza cha Liverpool, nyota huyo raia wa Ureno amepachika wavuni mabao saba na kuchangia moja.

Tangu aagane na Wolves na kuingia katika sajili rasmi ya Liverpool mnamo Septemba 2020, Jota amefunga magoli 20 kutokana na mechi 46 za mapambano yote. Hiyo ni rekodi ya kuridhisha zaidi ikizingatiwa kwamba jeraha baya la goti lilimweka mkekani kwa miezi mitatu msimu uliopita wa 2020-21.

Mabao 39 ya Liverpool baada ya michuano 13 pekee ni tisa zaidi kuliko idadi waliyojivunia walipotwaa taji la EPL mnamo 2019-20 na 10 zaidi kuliko magoli waliyokuwa wamejizolea kufikia hatua kama hii ligini msimu jana.

Liverpool walishindwa kuhifadhi ubingwa wa EPL mnamo 2020-21 baada ya uthabiti wa safu yao ya ulinzi kulemazwa na wingi wa visa vya majeraha. Lakini sasa wanasoka wao tegemeo wamerejea na kikosi kinazidi kuwa tishio kwa wapinzani wao. Miamba hao wameshinda mechi nane, kupiga sare mara nne na kupoteza mchuano mmoja pekee kati ya 13 iliyopita.

Tangu waambulie sare ya 2-2 dhidi ya Brighton katika EPL mwishoni mwa Oktoba, Liverpool wamepachika wavuni mabao 14 kutokana na mechi tano huku wapinzani wakitikisa nyavu zao mara mbili pekee.

MATOKEO YA EPL (Jumamosi):

Arsenal 2-0 Newcastle

Palace 1-2 Aston Villa

Liverpool 4-0 Southampton

Norwich City 0-0 Wolves

Brighton 0-0 Leeds United

You can share this post!

Haaland aweka rekodi ya kuwa mwanasoka mchanga zaidi...

Soi na Chepchirchir watwaa mataji ya La Rochelle Marathon...

T L