• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Soi na Chepchirchir watwaa mataji ya La Rochelle Marathon Ufaransa

Soi na Chepchirchir watwaa mataji ya La Rochelle Marathon Ufaransa

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Edwin Soi na Celestine Chepchirchir wameibuka washindi wa mbio za Marathon de la Rochelle mjini La Rochelle nchini Ufaransa, Jumapili.

Mshindi wa medali ya shaba mbio za mita 5,000 kwenye Olimpiki za Beijing mwaka 2008, Soi alikamilisha umbali huo wa kilomita 42 kwa saa 2:09:16. Ushindi huo ni wa kwanza kwa Soi baada ya kukamata nafasi ya sita kwa saa 2:14:52 katika mbio zake za kwanza za kilomita 42 wakati wa N Kolay Istanbul Marathon mwaka 2020.

Soi amekata utepe sekunde 14 mbele ya Mkenya mwenzake David Kiprono (2:09:30) nao Ivan Horodyskyy kutoka Ukraine (2:10:14), Muethiopia Azmeraw Mengist (2:11:47) na Mkenya Gilbert Masai (2:11:59) wakafunga nafasi tano za kwanza.

Kirwa alikuwa mbele baada ya kilomita tano za kwanza, Noah Kibet katika kilomita ya 10 na kilomita ya 15, Horodyskyy kilomita 21, Kirwa ya 25 kabla ya Soi kuchupa uongozini kutoka kilomita ya 30 hadi mwisho. Chepchirchir alitumia saa 2:23:38 kufika utepeni akifuatwa kwa karibu na Muethiopia Aberash Fayesa (2:25:32), Mkenya Judith Jerubet (2:26:43), raia wa Ukraine Yevheniya Prokofyeva (2:31:23) na Mkenya Winny Jepkorir (2:35:18) mtawalia.

Wakenya Emmanuel Oliaulo na Marion Kibor walitawala makala yaliyopita ya Rochelle Marathon mwaka 2019 yalipofanyika mara ya mwisho. Mbio za 2021 zilivutia watimkaji 4, 793.

You can share this post!

Liverpool waweka rekodi katika soka ya Ligi Kuu ya...

Krop na Jebitok wang’ara mbio za nyika za Kapsokwony

T L