• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Lukaku sasa andazi moto linalowaniwa na PSG na Manchester City

Lukaku sasa andazi moto linalowaniwa na PSG na Manchester City

Na MASHIRIKA

PARIS Saint-Germain wamejitosa katika vita vya kuwania huduma za mshambuliaji matata wa Inter Milan na timu ya taifa ya Ubelgiji, Romelu Lukaku ambaye pia anaviziwa na viongozi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Manchester City.

Lukaku anaingia kwenye rada za klabu hizo maarufu za bara Ulaya baada ya kushuhudia ufufuo wa makali yake akivalia jezi za Inter wanaonolewa sasa na kocha Antonio Conte.

Lukaku aliingia katika sajili rasmi ya Inter mnamo Agosti 2019 baada ya kuagana na Manchester United kwa Sh10.3 bilioni. Tangu ajiengue uwanjani Old Trafford, fowadi huyo wa zamani wa Everton amefungia Inter jumla ya mabao 54 kutokana na mechi 78.

Ni kuimarika kwa makali yake mbele ya malango ya wapinzani ambako kumevutia Man-City wanaopania kutafuta kizibo cha Sergio Aguero anayehusishwa na uwezekano mkubwa wa kuyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Barcelona mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

Kwa mujibu wa gazeti la Calciomercato nchini Italia, PSG wanahemea huduma za Lukaku kwa matarajio ya kujaza nafasi za Kylian Mbappe na Angel Di Maria ambao wanatarajiwa kuondoka ugani Parc des Princes mwishoni mwa msimu huu ili kumpisha nyota Lionel Messi anayetazamiwa kuagana na Barcelona na kuungana na Neymar Jr jijini Paris, Ufaransa.

Awali, PSG walipania kumtwaa chipukizi wa Borussia Dortmund, Erling Haaland ambaye kwa sasa anahusishwa na Manchester United na Chelsea.

Hata hivyo, gazeti la Mundo Deportivo linasisitiza kwamba kutua kwa Aguero kambini mwa Barcelona huenda kukamchochea Messi kusalia uwanjani Camp Nou kwa muda mrefu zaidi chini ya mwenyekiti mpya atakayechaguliwa na kikosi hicho mnamo Machi 2021. Aguero na Messi huchezea timu ya taifa ya Argentina.

Mkataba wa sasa kati ya Aguero na Man-City unatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu, kumaanisha kwamba yuko radhi kuanza mazunumzo na kikosi chochote kinacholenga kumsajili bila ada yoyote.

Japo anawaniwa pia na Olympique Lyon ya Ufaransa, huenda Aguero akawa radhi zaidi kurejea Uhispania ikizingatiwa kwamba amewahi kuhudumu kambini mwa Atletico Madrid.

Licha ya kukosa huduma za mvamizi mkuu, Man-City ambao kwa sasa wananolewa na kocha Pep Guardiola bado wanaselelea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa alama 50, tano zaidi kuliko nambari mbili Man-United ambao wamesakata mchuano mmoja zaidi kuliko Man-City waliowapiga Liverpool 4-1 katika mechi yao iliyopita ya EPL.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

Mwanasoka mstaafu Ronald Okoth ni balozi mpya wa kituo cha...

Mkongwe Harry Redknapp arejea Bournemouth kusaidia kazi ya...