• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Magnolia Girls Run kufanyika Novemba

Magnolia Girls Run kufanyika Novemba

NA RUTH AREGE

SHIRIKA la Rainbow of Magnolia-Fountains of Life, likishirikiana na Shirika la Riadha Kenya (AK), limeandaa makala ya pili ya mbio za barabarani kwa jina ‘Magnolia Girls Run’ kuchangisha fedha ambazo zinalenga kuwasaidia watoto maskini katika kaunti ya Kajiado.

Fedha hizi zinalenga kuwasaidia watoto wadogo kuwatoa katika ndoa za mapema, kuwaepusha tohara za wanawake na unyanyasaji nyumbani.

Mashindano hayo yananuiwa kuchangisha fedha za kusaidia kugharimia elimu ya wasichana nyumbani, kusaidia kujenga nyumba ya kulala ambayo itakuwa makazi yao. Pia, fedha hizo zitagharamia afya ya wasichana wenye mahitaji spesheli ya matibabu.

Mwaka 2015, wasichana 12 wa kati ya umri wa miaka 11-13, walikimbilia eneo hilo la Rainbow of Magnolia-Fountains of Life katika kaunti ya Kajiado baada ya kudhulumiwa. Mradi huo kwa sasa umekuwa nyumbani kwa wasichana na wavulana wengi ambao wanadhulumiwa.

Kulingana na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Robert Saruni, ameomba wakenya kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizi, kuwasaidia watoto hawa kuishi maisha ya kawaida.

“Kama njia mojawapo ya kuchangisha fedha, shirikisho hilo limeandaa mbio za barabarani kwa jina  ‘Magnolia Girls Run’. Mbio hizo zitafanyika tarehe 27 mwezi Novemba mwaka huu katika barabara kuu ya Lang’ata mjini Nairobi.”

“Watakaoshiriki watakimbia kilomita tano na 10. Kama shirika tunatafuta kufuata taratibu zote zinazofaa na tayari tumekusanya kamati ya maandalizi ambayo itaongoza vipengele vyote vinavyohitajika kwa utekelezaji wa mbio hizi,” alisema Saruni.

Saruni aidha nasema, mbio hizi zinalenga washiriki 10,000 kutoka kote nchini pamoja na mashirika ambayo tayari yameshirikiana nao.

Kwa upande wa Makamu Mwandamizi wa Rais wa AK Paul Mutwii, aliunga mkono mradi huo na kuahidi kushirikiana nao kuwasaidia watoto hao kujenga maisha yao ya baadaye.

“Watu ambao wananyanyasa watoto wadogo sio watu tena bali ni wanyama au zaidi ya hapo. Watu kama hao hawafai kuishi na sisi kwenye jamii. Yeyote ambaye alianza mradi huu nampongeza sana na anafaa kupewa kongole,” alisema Mutwii.

“Serikali kuu pia inafaa kuhusishwa kwenye miradi kama hii, kusaidia vizazi vya kesho. Hili ni jambo ambalo limenigusa sana na nitashirikiana nanyi kuona kuwa mradi huu umeenda sawa. Ninaomba Wakenya kujitokeza kwa wingi ilikuchangisha fedha,” aliongezea Mutwii.

Usajili wa kushiriki mbio hizo utaanza wiki ijayo. Kila mmoja ambaye anataka kushiriki anatarajiwa kujisajili na Shilingi 1,500. Shirika hilo linalenga kukusanya Sh10 milioni.

  • Tags

You can share this post!

Faida anazozipata mtu kwa kula tanipu

Hatimaye dalili zaonekana za msimu mpya Ligi Kuu ya Kenya

T L