• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 1:02 PM
Majeraha yalemaza Ufaransa huku Benzema akiungana na Kante, Pogba, Nkunku na Kimpembe mkekani

Majeraha yalemaza Ufaransa huku Benzema akiungana na Kante, Pogba, Nkunku na Kimpembe mkekani

NA MASHIRIKA

UFARANSA wamepata pigo la kukosa huduma za mvamizi na mwanasoka bora zaidi ulimwenguni, Karim Benzema, katika vita vya kutetea ubingwa wao wa Kombe la Dunia nchini Qatar.

Benzema, 34, amekuwa na tatizo la paja la kushoto tangu Oktoba na aliwajibikia Real Madrid kwa dakika zisizozidi 30 kutokana na mechi sita zilizopita. Alinyanyua Ballon d’Or mwaka huu baada ya kuongoza waajiri wake kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Nyota huyo aliyejeruhiwa tena akishiriki mazoezi nchini Qatar, sasa atakuwa mkekani kwa kipindi cha majuma matatu.

“Namsikitikia sana Benzema aliyelenga kufanya makuu kwenye fainali hizi,” akasema Didier Deschamps ambaye pia atakuwa bila mshambuliaji Christopher Nkunku na viungo Paul Pogba na N’Golo Kante kutokana na majeraha.

Ufaransa waliopepeta Croatia 4-2 kwenye fainali za 2018 nchini Urusi, watafungua kampeni za Kundi D dhidi ya Australia hapo kesho kabla ya kuonana na Denmark (Novemba 26) kisha Tunisia (Novemba 30).

Deschamps aliyetarajiwa kuita Anthony Martial kambini, amesema hatajaza pengo la Benzema. Mkufunzi huyo atakosa pia maarifa ya beki mzoefu wa Paris Saint-Germain (PSG), Presnel Kimpembe, aliyejiondoa kikosini wiki moja iliyopita kutokana na jeraha la paja.

Nafasi ya Kimpembe ilichukuliwa na Axel Disasi huku Randal Kolo Muani akijaza pengo la Nkunku. Beki Raphael Varane aliyekosa mechi tano zilizopita za Manchester United, bado hajapona kabisa jeraha la paja.

“Licha ya pigo hili jipya, nina imani tele kwa kikosi changu. Tutajitahidi kadri ya uwezo kukabiliana na kibarua kizito kinachotusubiri,” akasema Deschamps aliyeongoza Ufaransa kukomoa Brazil 3-0 kwenye fainali za Kombe la Dunia 1998 akivalia utepe wa nahodha.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA 2022: Jacob ‘Ghost’ Mulee...

Qatar yapigwa na Ecuador na kuwa timu ya kwanza kuwahi...

T L