• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 3:09 PM
Makala ya spoti- Bandari FC

Makala ya spoti- Bandari FC

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

NI mambo gani ambayo Bandari FC, klabu ya pekee ya jimbo la Pwani kushiriki kwenye Ligi Kuu ya FKF imeweza kufanikiwa msimu uliomalizika mbali na  kukamilisha mechi zao za ligi hiyo katika nafasi ya tatu?

Washika dau na wapenzi wa klabu hiyo wanaamini mbali na kufanikiwa kukamilisha ligi hiyo kwenye nafasi ya tatu lakini pia imepata fursa ya kuwatengeneza chipukizi kadhaa ambao nao wamesaidia pakubwa kuifanya Bandari kuwa mojawapo ya timu kubwa nchini.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Cosmos FC, Aref Baghazallay anasema mafanikio makubwa Bandari imepata ni kutokana na kocha mkuu Andre Cassa Mbungo kuamua kuwachezesha wanasoka chipukizi ambao hapo awali alikuwa hakuwapa nafasi ya kucheza.

Wanasoka hao chipukizi ambao wamesajiliwa kutoka timu yao ya Bandari Youth ama timu nyingine, Mbungo alikuwa akiwaweka katika benchi la wachezaji wa akiba ama kutowapa nafasi ya kuwamo kwenye orodha ya wachezaji wa akiba.

“Tulifurahikia kumuona Mbungo akikubaliana na maoni ya washika dau na mashabiki ya kumtaka kuwachezesha baadhi ya wanasoka waliokuwa wanaozea katika benchi la wachezaji wa akiba ama kuachwa kabisa katika orodha ya wanasoka 18 wa siku za mechi; matokeo ambayo yalisaidia kuvumbua wachezaji wenye vipaji,” akasema Baghazally.

Beki wa Bandari FC, Siraj Mohamed aliyechaguliwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Harambee Stars baada ya mashabiki wa timu hiyo kulilia hilo miaka kadhaa…PICHA/ABDULRAHMAN SHERIFF

Mkurugenzi huyo wa Cosmos FC amaesema jambo kubwa ambalo kocha Mbungo alilitekeleza na ambalo liliisaidia Bandari FC kufanya vizuri hasa kwenye mechi za mwisho za msimu ni kule kuwapa nafasi chipukizi waliothibitisha wataweza kuihami timu wanapotakiwa kufanya hivyo.

Alisema wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza alichokiamini mkufunzi huyo walionekana wamechoka na hivyo uamuzi wake wa kuwapa nafasi wale waliokuwa wakisubiri nafasi ya kucheza ulisaidia kwani wale waliocheza walithibitisha ubora wao na kuisaidia timu kufanya vizuri.

Miongoni wa wanasoka waliothibitisha kuwa wanaweza kuihami timu yao hiyo ya Bandari mbali na kuinua vipaji vyao ni pamoja na kiungo mkabaji Dennis Magige, beki Hassan Iddi na Swaleh Chacha ambao kuchezeshwa kwao kumeonyesha kuwa Bandari inao wanasoka wanaoweza kuitumikia timu hiyo kwa miaka kadhaa ijayo.

Magige, Iddi na Chacha walipopewa nafasi ya kushika namba katika kikosi hicho, walithibitisha ubora wao kwa kucheza kwa ari na moyo wa kuipenda timu na kuhakikisha kuingizwa kwao timuni hakukuwa kwa bahati mbaya bali wanastahili kuichezea kama walivyo wanasoka wengine.

Ni jambo la kufurahisha kuona wakati ligi ilipokuwa inaingia kikomoni, beki wa timu hiyo Siraj Mohamed ambaye alililiwa na mashabiki wengi wakimpigania achaguliwe katika kikosi cha timu ya taifa, aliitwa katika kikosi cha kocha wa Harambee Stars, Jacob ‘Ghost’ Mulee akijumuika na mwenzake Abdalla Hassan.

Kocha Mbungo amesema ana imani wanasoka wake wengine nao pia wakati ukifika watachaguliwa kwenye timu ya taifa. Mkufunzi huyo hakutaka kuwataja majina lakini mashabiki wamekuwa wakimtaja winga wa timu hiyo, Darius Msagha kuwa miongoni mwa wachezaji wanaostahili kuitwa katika kikosi cha Stars.

Ni jambo lilowatia moyo mashabiki wa Bandari na wale wa soka wa jimbo la Pwani kumsikia Siraj akieleza kuwa atafanya bidii kuhakikisha anawaridhisha wakuu wa benchi la ufundi la Stars ilia pate kubakia katika timu katika mechi zake za kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Mashabiki wa Bandari wana hamu kubwa ya timu yao hiyo kubeba taji la Ligi Kuu kwani imepita miaka 56 tangu timu ya jimbo hilo la Pwani ya Feisal FC kuwa ya pekee kushinda kombe la Ligi Kuu ya Kenya mnamo mwaka 1965. 

  • Tags

You can share this post!

Kamket alala seli tena Lempurkel akijitetea

Wazee wakemea mzozo wa ugavana Wajir