• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:02 PM
Makao makuu ya judo Afrika sasa ni Nairobi

Makao makuu ya judo Afrika sasa ni Nairobi

Na AYUMBA AYODI

SHIRIKISHO la Judo Afrika (AJU) limehamisha makao yake makuu kutoka Antananarivo, Madagascar hadi Nairobi.

Katika barua kwa Waziri wa Michezo Amina Mohamed, Rais wa AJU Thierry Siteny alisema kuwa kuhamishwa kwa afisi hizo kutaharakisha ukuaji wa judo barani Afrika kwa sababu Nairobi ipo katikati.

Siteny alisema kuwa hatua hiyo pia itampa mwenyekiti wa AJU Shadrack Maluki kutoka Kenya muda mzuri wa kuendesha mchezo huo mbali na kuweka mikakati ya kuwa na kituo cha maendeleo cha mchezo huo nchini Kenya.

Kituo hicho kitahudumia maeneo ya Mashariki, Kati na Afrika ya Kusini.

Siteny alisema kuwa amependekeza wafanyakazi wawili kuwa katika sekretariati hiyo ambapo gharama zote zitalipwa na AJU.

“Tumechagua Kenya kwa sababu ya mchango mkubwa kutoka kwa serikali yake katika kukuza mchezo wa judo,” alisema Siteny.

“Ningependa kutoa heshima zangu kwa Wizara ya Michezo kwa juhudi imefanya katika kuendeleza judo licha ya changamoto za ugonjwa wa Covid-19.”

Siteny alisema kuwa AJU inaipa uzito ukuzaji wa judo barani Afrika na, Maluki ataweza kusimamia shughuli vyema akiwa karibu na makao hayo makuu.

Maluki, ambaye ni rais wa Shirikisho la Judo Kenya, alipongeza hatua ya makao makuu ya AJU kuwa Kenya akisema ni habari za kutia moyo kwa Kenya na Afrika.

Maluki alisema kuwa afisi jijini Nairobi zitaharakisha kuwepo kwa kituo cha eneo hili mbali na kuleta mashindano ya kifahari ya Shirikisho la Kimataifa la Judo (IJF) ya Grand Slam jijini Nairobi.

Mashindano hayo yatafahamika kama Safari Judo Grand Slam. Yanatarajiwa kuandaliwa kabla ya 2022 kukamilika.

Grand Slam ni ya tatu kwa ukubwa katika mchezo wa judo baada ya Olimpiki na mashindano ya dunia. Maluki alisema kuwa tarehe za mashindano hayo zitatangazwa baadaye.

Wakati huo huo, Kenya imechaguliwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya chipukizi na makadeti 2022.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

You can share this post!

Meja acheka na nyavu mara mbili kuisaidia AIK kutoka sare...

Teknolojia mpya ya kupima Covid-19 kupiga jeki utalii,...

T L