• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Makocha wa voliboli kutoka Brazil sasa wachukua usukani wa Malkia Strikers

Makocha wa voliboli kutoka Brazil sasa wachukua usukani wa Malkia Strikers

Na GEOFFREY ANENE

MAKOCHA kutoka Brazil wamechukua usukani wa timu ya taifa ya voliboli ya wanawake ya Kenya maarufu kama Malkia Strikers.

Kocha mkuu wa klabu ya Osasco nchini Brazil Luizomar de Moura ametwikwa majukumu ya kocha mkuu wa Malkia Strikers akisaidiwa na kocha wa zamani wa timu ya chipukizi ya Brazil Jefferson Arosti (naibu kocha), mkufunzi wa mazoezi ya viungo Marcelo Vitorino de Souza naye Roberto Opice Neto ni meneja wa timu hiyo.

Malkia Strikers imepigwa jeki na makocha hao wanne kutoka Brazil inapojiandaa kurejea kwenye Olimpiki baadaye mwaka huu baada ya kukosa makala matatu yaliyopita.

Taarifa kutoka Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K) zimesema Jumanne kuwa Wabrazil hao watasaidia mabingwa hao wa Afrika kujiandaa vyema kwa Olimpiki zitakazofanyika mjini Tokyo mnamo Julai 23 hadi Agosti 8 mwaka huu.

“Makocha wa Brazil wamekuja kupiga jeki timu ya Kenya kupitia mradi wa Shirikisho la Voliboli Duniani (FIVB) kwa ushirikiano wa Shirikisho la Voliboli Kenya (KVF) na NOC-K,” NOC-K imeongeza na kufichua kuwa mazungumzo ya kina yalifanywa kati ya mashirika hayo matatu miezi mingi iliyopita.

“Watafanya kazi na timu hiyo hadi mwisho wa mwezi huu. Wako hapa kuangalia hali ya timu ilivyo na jinsi makocha wanafanya kazi,” kamati hiyo ilifichua.

Lengo kubwa, NOC-K inasema, ni kusaidia wawakilishi hao wa pekee wa Afrika kwenye Olimpiki kuimarisha mchezo wao na matokeo hata baada ya Olimpiki ili kibadilisha fikra ya ulimwengu kuhusu unavyochukulia voliboli ya wanawake kwenye ulingo wa dunia.

Benchi ya kiufundi ya Malkia Strikers ikiongozwa na Paul Bitok itafikiwa na mradi huu unaolenga pia kuwainua. Wachezaji 16 wa timu hiyo watasafari nchini Brazil mwanzo wa mwezi Mei kushiriki kambi ya mazoezi ya siku 45 pamoja na michuano ya kujipima nguvu.

You can share this post!

KRU kuwa mpatanishi wa amani kati ya Pokot na Marakwet,...

Wakazi wa mitaa ya mabanda Nairobi wahangaika kupata maji