• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
Malkia Strikers yapigwa na Serbia kwenye Kundi A voliboli katika Olimpiki

Malkia Strikers yapigwa na Serbia kwenye Kundi A voliboli katika Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

VICHAPO vinazidi kuwa vikali kwa timu ya taifa ya voliboli ya kinadada ya Kenya baada ya kukung’utwa na mabingwa wa dunia Serbia kwa seti 3-0 ukumbini Ariake Arena jijini Tokyo, Japan mnamo Alhamisi.

Kenya inayonolewa na raia wa Brazil Luizomar de Moura akisaidiwa na Mkenya Paul Bitok na raia mwingine wa Brazil Jefferson Arost, ilitoa Serbia kijasho seti ya kwanza kabla ya kuipoteza kwa alama 25-21 ndani ya dakika 25.

Wawakilishi hao wa Bara Afrika walipotea katika seti ya pili wakipigwa 25-11 katika dakika 23 kabla ya kupoteza seti ya tatu kiheshima 25-20 ndani ya dakika 26.

Brankica Mihajlovic alifungia Serbia alama nyingi na pia katika mechi hii (17) naye Sharon Chepchumba akawa mfungaji bora kwa upande wa Kenya kwa alama 12.

Malkia Strikers ilijibwaga uwanjani ikiuguza vichapo vya 3-0 mikononi mwa wenyeji Japan (25-15, 25-11, 25-23) hapo Julai 25 na pia kupokea dozi sawa na hiyo kutoka kwa Korea Kusini (25-14, 25-22, 25-24) Julai 27.

Kenya imesalia na michuano miwili katika Kundi A; dhidi ya Dominican (Julai 31) na Brazil (Agosti 2).

Serbia inaongoza kundi hili kwa alama tisa baada ya kushinda michuano yake mitatu ikifuatiwa na Brazil na Korea Kusini (sita kila moja).

Japan ina alama tatu kutokana na mechi mbili nayo Dominican ni ya tano kwa alama mbili. Kenya bado haijapata alama.

Dominican na Kenya zimesakata mechi tatu. Timu nne za kwanza zitaingia robo-fainali.

You can share this post!

Msimamo wa medali za Olimpiki 2020

Rais awaongoza Wakenya kumwomboleza mumewe waziri Amina...