• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 7:52 PM
Man-City waponda Newcastle United ugani Etihad na kurejea kileleni mwa jedwali la EPL

Man-City waponda Newcastle United ugani Etihad na kurejea kileleni mwa jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City walirejea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kuweka hai matumaini ya kuhifadhi taji la kipute hicho msimu huu baada ya kuponda Newcastle 5-0 mnamo Jumapili ugani Etihad.

Masogora hao wa kocha Pep Guardiola sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 86, tatu zaidi kuliko nambari mbili Liverpool ambao pia wametandaza mechi 35.

Man-City walichuma nafuu kutokana na kuteleza kwa Liverpool walioambulia sare ya 1-1 dhidi ya Tottenham Hotspur mnamo Mei 7, 2022 ugani Anfield na kuimarisha zaidi tofauti yao ya alama. Kinyume na Liverpool ambao wamefunga mabao 87 na kuokota mpira kimiani mara 23, Man-City wametikisa nyavu za wapinzani wao mara 89 na kuruhusu wapinzani kuwafunga mabao 21 pekee.

Licha ya kuanza mechi kwa matao ya juu, Newcastle walipoteza nafasi ya kujiweka kifua mbele kupitia kwa Chris Wood. Man-City walifungua karamu ya mabao kupitia kwa Raheem Sterling aliyefunga mawili huku magoli mengine yakijazwa kimiani na Aymeric Laporte, Rodri na Phil Foden.

Kichapo hicho kilisaza Newcastle katika nafasi ya 13 jedwalini kwa alama 43 sawa na Aston Villa na Brentford. Man-City walishuka dimbani wakilenga ushindi ambao pia ungewawezesha kuweka kando maruerue ya kung’olewa na Real Madrid kwenye nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu. Walikung’uta Newcastle 4-0 katika mkondo wa kwanza wa ligi msimu huu ugani St James’ Park mnamo Disemba 2021.

Miamba hao wamepoteza mechi moja pekee kati ya 29 zilizopita dhidi ya Newcastle huku wakishinda 13 zote dhidi ya kikosi hicho katika uwanja wao wa nyumbani wa Etihad. Newcastle ambao sasa wamefungwa na Man-City mabao 22 kutokana na mechi sita zilizopita ligini, waliangusha mabingwa hao watetezi wa EPL mara ya mwisho mnamo Septemba 2000 kwa 1-0.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Hofu idadi ya punda kupungua kwa kuendelea ‘kudhulumiwa’

‘Azimio kupoteza viti vikuu kutokana na ushindani...

T L